Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 13 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 148 | 2026-04-21 |
Name
Jacqueline Andrew Kainja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa elimu ya kutosha kwa wananchi wanaoishi maeneo ya karibu na Hifadhi ya Ugalla Wilaya ya Urambo?
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla mwaka 2019, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi ambapo jumla ya mikutano ya hadhara 60 ilifanyika na kuwafikia wananchi 10,000 pamoja na vipindi 505 vya elimu ya uhifadhi vilivyowafikia wananchi 58,100.
Mheshimiwa Spika, pia, hifadhi ilishiriki kutoa elimu ya uhifadhi kwenye mikutano ya vijiji 102 na kuwafikia wananchi 8,000 na kutoa elimu ya uhifadhi kwenye vipindi 160 kwenye shule mbalimbali katika Wilaya ya Urambo, Kaliua na kuwafikia wanafunzi 15,000.
Mheshimiwa Spika, vilevile, hifadhi imekuwa na program ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa njia ya sinema, ambapo jumla ya mikutano kupitia njia za sinema 49 ilifanyika na kuwafikia wananchi 8,500. Katika kuimarisha mahusiano na jamii iliyopo jirani na hifadhi, hifadhi iliandaa ziara mbili za elimu ya uhifadhi kwa njia ya kutembelea hifadhi ambazo zilihusisha wananchi 130 na kuratibu michezo miwili iliyowashirikisha wananchi 470.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka ujao, hifadhi imejipanga kupanua wigo zaidi wa kutoa elimu ya uhifadhi kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii, hususan vijana na wanafunzi ili kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko ya tabia chanya juu ya shughuli za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, jumla ya vipindi 112 vimepangwa kufanyika vikilenga kufikia zaidi ya wananchi 11,860 ikijumuisha mikutano ya hadhara, mikutano ya vijiji, vipindi mashuleni, maonesho, maonesho ya sinema, ziara ya kutembelea hifadhini, michezo na vikao. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved