Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 9 | Defence and National Service | Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa | 100 | 2026-04-15 |
Name
Onesmo Merdson Mnkondya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbozi
Primary Question
MHE. ONESMO M. MNKONDYA aliuliza: -
Je, lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi waliopisha eneo la JKT Itaka?
Name
Rhimo Simeon Nyansaho
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kuzungumza mbele ya Bunge lako, ninaomba nitumie wasaa huu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Mbunge, lakini pia, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Onesmo Mnkondya, Mbunge wa Mbozi, kwanza kwa namna anavyofuatilia suala la malipo ya fidia ya wananchi waliopisha eneo letu la JKT Itaka lililopo Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inakiri kufanya uthamini katika maeneo ya Kikosi cha 845 KJ kilichopo Itaka JKT, ili kulipa fidia kwa wananchi wanaotarajia kupisha maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya jeshi letu. Uthamini huo ulifanyika Mwaka 2022 na kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali (Chief Valuer) mwaka wa fedha 2023/2024 ukiuhusisha maeneo ya Vijiji vya Sasenga, Mbozi na Itewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla kuu ya gharama ya fidia kulingana na Mthamini Mkuu wa Serikali ni shilingi 5,715,942,200. Kati ya fedha hizo zimegawanywa katika makundi matatu ambapo, kundi la kwanza litalipwa shilingi 3,491,271,800. Hii ni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wapatao 312 katika Kijiji cha Sasenga, shilingi 74,358,600 inawalipa wananchi wanne katika Kijiji cha Mbozi na mwisho ni shilingi bilioni 2.15 ambayo hii inawalipa wananchi 150 katika Kijiji cha Itewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majedwali ya uthamini au valuation ya kulipa fidia yamewasilishwa tayari Hazina (Wizara ya Fedha), ili taratibu za uhakiki na ulipaji ziendelee. Aidha, Wizara inaendelea kuwasiliana kwa karibu na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha wananchi wetu wanalipwa fidia zao kulingana na uthamini uliofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wananchi hawa waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho Serikali inashughulikia suala lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved