Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 4 | Planning and Investment | Ofisi ya Rais: Mipango na Uwekezaji | 25 | 2026-04-08 |
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. EMANUEL Q. NUWAS K.n.y. MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isipitie upya Mkataba wa Shamba la Basotu la mwekezaji Ngano Limited lenye ukubwa wa ekari 43,000 ambalo limekuwa pori?
Name
Dr. Pius Stephen Chaya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shamba la Basotu ni miongoni mwa mashamba sita yaliyokuwa yanamilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (National Agriculture and Food Corporation) ambayo yalisitishwa ubinafsishwaji wake mwaka 2007 kutokana na maamuzi ya Baraza la Mawaziri kupitia Waraka Na. 23 wa mwaka 2003 na kubaki chini ya Msajili wa Hazina yakisubiri maamuzi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba niweke taarifa sahihi kwamba katika Shamba ya Basotu lenye ukubwa wa ekari 13,295 hakuna mkataba wowote na mwekezaji, bali shamba hilo linamilikiwa na Serikali kupitia Msajili wa Hazina na kwa sasa liko chini ya uangalizi wa Halmashauri ya Hanang, ambayo imekuwa ikikodisha kwa wakulima wadogo wadogo na baadhi ya taasisi za Serikali kwa kilimo cha mazao ya muda mfupi, kama vile mahindi na alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali inaendelea kutafuta mwekezaji mkubwa ili aweze kuwekeza kwenye kilimo cha ngano kwa lengo la kukuza ajira, uchumi wa watu wa Manyara na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji Ngano Limited aliuziwa na Serikali mashamba matatu. Setchet ekari 15,825, Murjanda ekari 15,750, na Gidagamowd ekari 12,900 kwa ajili ya kilimo cha ngano kupitia iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma mwaka 2003. Hata hivyo, mwekezaji huyo hajaweza kuwekeza kama ambavyo mkataba wa mauziano ulivyomtaka kwani ni eneo dogo tu ndilo linalolimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hii, tayari ofisi yetu kupitia TISEZA ilishapokea maelekezo ya mamlaka kufanya tathmini ya tija ya mwekezaji huyu ili maamuzi sahihi yaweze kuchukuliwa yatakayokuwa na tija kwa pande zote mbili kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ngano nchini na kuzalisha ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na TISEZA imeendelea kufanya ufuatiliaji na tathmini kwa wawekezaji wote nchini ambao wamekabidhiwa mashamba au viwanda kwa ajili ya kuwekeza kwa kuongeza tija na kuendeleza shughuli za uzalishaji kama ilivyokusudiwa. Hivyo, Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki na za haraka pale inapobainika kuwa masharti ya mikataba hayatekelezwi na mwekezaji ili kulinda maslahi ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved