Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 2 Sitting 6 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 108 2026-02-03

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na wanyama waharibifu na wakali wanaotoka Hifadhi ya Ngorongoro na Ziwa Manyara – Karatu?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kwa unyenyekevu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu Wilaya ya Karatu, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuongeza doria pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia kwa kutumia ndege nyuki; kuanza ujenzi wa Kituo cha Askari katika Kijiji cha Lostete kilichopo mpakani mwa hifadhi; na kutumia Askari wa Vijiji (VGS) wanaoshirikiana na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali itajenga uzio wa umeme wenye urefu wa kilometa 15 ili kukinga na kuzuia tembo na wanyamapori wengine kuingia kwenye maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, Serikali imeandaa Mkakati mpya wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migogoro baina ya Binadamu na Wanyamapori wa miaka 10 kuanzia 2025/2026 hadi 2035/2036. Mkakati huu utatekelezwa kwa ushirikiano na Wizara za kisekta ikiwemo TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha kuwa jitihada za kupunguza changamoto hii zinafanyika kwa pamoja na kwa ufanisi mkubwa.