Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 2 | Sitting 2 | Community Development, Gender and Children | Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum | 35 | 2026-01-28 |
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kuweka Sharti la Kisheria la Watoto wakubwa kutunza wazazi wao wasiojiweza?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, ninaomba kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya siku ya leo, lakini pili ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoionesha juu yangu kwa kuendelea kuniteua kama Naibu Waziri, wakati huu kwa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili niweze kumsaidia Field Marshal wetu Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba sasa nijielekeze kwenye swali. Serikali inatambua umuhimu wa familia na jamii kuchukua jukumu la kulea wazee, na huu ndiyo msingi wa mila na desturi zetu Watanzania. Jukumu hili ni msingi unaojengwa katika hatua za awali katika malezi na makuzi ya watoto wetu.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma na matunzo kwa wazee, Serikali imefanya mapitio na kutunga Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2024. Sera hiyo inatoa wajibu kwa familia na jamii kusimamia matunzo ya wazazi. Sera hii imeweka msisitizo wa kuimarisha mfumo wa kisheria utakaolinda na kuendeleza wazee ambao pamoja na mambo mengine, utawezesha uwajibikaji wa jamii na watoto kuwatunza wazee wao. Kwa sasa Serikali ipo kwenye hatua ya kuwashirikisha wadau ili kutoa maoni juu ya umuhimu na masuala muhimu ya kuzingatiwa katika sheria hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kutoa wito kwa wazazi kuwekeza kwenye malezi ya watoto na siyo matunzo peke yake, kwani inaendeleza ukaribu na muunganiko imara kati ya wazazi na watoto. Mzazi anapobeba jukumu la malezi na matunzo ya watoto wake kikamilifu, hujenga msingi imara kwa mtoto kumhudumia mzazi wake anapozeeka. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved