Supplementary Questions from Hon. Bakari Bakari Shingo (5 total)
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nina swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo langu la Ukonga, hasa Halmashauri yetu Jiji la Dar es Salaam moja ya mambo yaliyopelekea halmashauri ikahamisha utaratibu wa kukopesha moja kwa moja ni baadhi ya watumishi wa halmashauri na baadhi ya Madiwani walisemwa kwamba wamekuwa wakitumia mlango wa nyuma kujikopesha, lakini pia kuwepo na vikundi ambavyo sasa vimekopeshwa zaidi ya mamilioni na vimetajwa kuwa havionekani.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni kuwa; je, kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa na kodi zetu, ni kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuyataja hadharani hayo makundi ama hivyo vikundi vilivyokopa ambavyo sasa havionekani, sambamba na baadhi ya watumishi wa halmashauri ambao siyo waaminifu waolijingiza katika mtego huu ambao leo unapelekea halmashauri zetu kuhamisha Mfuko huo kupeleka kwenye benki, benki ambazo zinasababisha tushindwe kupata mikopo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Naibu wangu ameyatoa, kama alivyosema, tulikuwa na kikao na benki hizi. Kilichotokea ni kwamba, kweli kwenye majiji kuna fedha nyingi ambazo hazijakopeshwa uki-compare na kwenye halmashauri za wilaya na miji. Shida iliyopo, kutokana na maelezo waliyotupa benki; la kwanza, ni kweli kwamba walikuwa na masharti magumu, lakini kwa sasa sharti linalotakiwa kwa mtu kwa kikundi kukopa ni wale wanakikundi kuwa na NIDA.
Mheshimiwa Spika, nini kimesababisha sasa majiji yawe na fedha nyingi; wamesema, ni kwa sababu wale wanaounda vikundi walioko Dar es Salaam kwa mfano wanakutana kimjini mjini, kwa hiyo hawawezi na inakuwa ngumu sana kupata kikundi kimoja cha watu ambao wanaweza kukopeshwa kwa wakati huo. Hii ni kwa sababu, huyu ametoka Segerea, mwingine ametoka Ubungo, mwingine tena ametoka Kawe na wanakutana Kariakoo kwenye biashara. Wakiwa pale kila mtu hajui huyo mwenzake ametokea wapi.
Mheshimiwa Spika, proposal ya benki ni kwamba, ikiwezekana tuwape mikopo individuals kama tunavyofanya kwa walemavu; lakini tuwe na condition moja kwamba huyu individual tunayempa mkopo atuhakikishie kwamba kwanza ana biashara, ana leseni ya biashara; lakini pili, ataweza ku-employ angalau watu watatu kwenye ile biashara kutokana na mkopo tunaowapa.
Mheshimiwa Spika, kama hii itafanyika, kitu cha kwanza zile bilioni zilizolala kule benki zitatoka. Kitu cha pili, tutaona kwamba tume-create ajira kwa vijana ambao ni moja ya vitu ambavyo tunaviangalia sana kwenye fedha hii. Kwa hiyo Bunge lako hili ninaomba lielewe kwamba, tutakwenda kuona namna ya kubadilisha ule mwongozo na kukubali kwamba tuwe na pilot ya majiji ya kutoa mikopo kwa individuals ambao watatuhakikishia kwamba wata-create ajira kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, nimeomba nisimame nitoe ufafanuzi huu na kushukuru sana.
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Ukonga kuna Mradi wa Yangeyange, ambao ni mategemeo makubwa kwa wananchi wa Kata ya Pugu, Buyuni, Chanika na Zingiziwa, na pia ni mradi ambao unaonekana umekamilika, lakini hatujawahi kunufaika nao kwa sababu mara nyingi unaripotiwa kuwa na breakdown. Ninaomba nitambue shida ni viwango vya mabomba vilivyotumika pale viko chini, ama utalaamu ni mdogo, ama ni nini? Maana nilikuwa ziarani hata jana, bado tuna shida na tulikuwa tunaambiwa mradi ule una tatizo. Ninaomba nipate ufafanuzi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Bakari, kwa muda mfupi amekaa jimboni kwake, lakini ameshabaini baadhi ya changamoto hasa zinazolenga akina mama. Sisi kama Serikali tutaendelea kufanya kazi na Waheshimiwa Wabunge ili kuendelea kutatua changamoto za wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kupokea changamoto hii, na pia ninamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji atume timu iende kuukagua mradi huo, ije na tathmini ya nini kimefanyika, na wapi kuna tatizo? Kama kuna tatizo katika utekelezaji wa mradi, tuchukue hatua kulingana na changamoto ambazo zitabainika baada ya timu hiyo kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninakuhakikishia kwamba tutampatia jibu Mheshimiwa Mbunge kulingana na taarifa itakayopatikana.
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inaandaa mpango kwa ajili ya bima za afya. Swali langu lilikuwa linazungumzia kipindi hiki ambacho bima hiyo ya afya kwa wote haijaanza kukamilika, na huku tukijua kwamba nyuma kuna sera ya wazee kuhudumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu, kuna wazee kadhaa wameshindwa kupata hiyo huduma. Swali langu linasimama kwamba, hawana sifa ya kupata huduma hiyo wakati tukisubiri mpango huo wa Bima ya Afya kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Ukonga Mheshimiwa Bakari Bakari kwa kuwa kinara wa kutetea afya za akina mama wa Tanzania ili waweze kujifungua na kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya Bima ya Afya kuanza, Serikali ilikuwa na utaratibu maalum ambao wagonjwa hawa wa makundi maalum wakiwemo wajawazito, akina mama, watoto, na wazee walikuwa wanagharamiwa matibabu na Serikali bure kwa kupelekewa vifaa na kwa kupewa msamaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa mwaka kuwahudumia wagonjwa hawa kwa kutoa msamaha katika hospitali zetu. Wanapewa vipimo, wanapewa matibabu, wanajifungua kwa gharama za hospitali. Hii ndiyo imepelekea vifo vya mama na mtoto kupungua katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Suluhu Hassan ambaye aliamua kuwekeza kwenye idara hii ya mama na mtoto. Tumeona vifo vikipungua kwa zaidi ya 80%. Vifo vimetoka 556 kwa vizazi hai 100,000 mpaka vifo 104 kwa vizazi hai 100,000, hali iliyopelekea mpaka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Suluhu Hassan kutunukiwa tuzo ya Goal Keeper Award na Gates Foundation ambayo haijawahi kutokea kwa Rais yeyote mwananamke duniani kupewa tuzo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea Rais yeyote Afrika kupewa tuzo hii. Yeye akiwa ni Rais wa kwanza Tanzania kupewa tuzo hii kwa sababu kwa moyo wa dhati kabisa amewekeza katika kumhudumia mama na mtoto ili kupunguza vifo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo malengo mkakati, ifikapo mwaka 2030 tunataka kupunguza vifo vya mama na mtoto mpaka kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000. Ndiyo maana tumekwenda kwa Bima ya Afya kwa Wote ili sasa kuwa na huduma bora zaidi kwa ajili ya akina mama waweze kujifungua salama na watoto wao waendelee kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu msingi wake ulitokana na ujenzi huo wa barabara ambapo ujenzi huo umepelekea kuwa na mafuriko na Mheshimiwa Waziri analijua hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Mombasa kulikuwa na kalavati la asili pale lenye ukubwa wa sentimita 60, sasa hivi ujenzi huu wameenda kuweka kalavati lenye ukubwa kama sentimita 90 ama 120 ambayo imepelekea mafuriko, ndiyo ambayo swali langu la msingi lilivyokuwa linaelekea hivyo. Kumekuwa na mafuriko sasa Wizara iniambie inafanyaje kudhibiti yale mafuriko yasiende kuingia kwenye makazi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na tukio hilo pia lipo katika msikiti wa mashine ya maji kwamba pale tulikuwa na kalavati kubwa lenye ukubwa wa zaidi ya sentimita 120 sasa hivi ile njia imefungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo kitendo cha kufunga na barabara imepanda juu kumesababisha pia mafuriko yanaingia kwenye misikiti na majengo ya wakazi eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, hapo mwisho wa stendi ya mwendokasi palikuwa na kalavati, kalavati lile limeondelewa pakajengwa stendi kwa hiyo maji yamekuwa mafuriko na yanaelekea kwenye makaburi ya Kiltex ambavyo hivi ninavyozungumza inawezekana hata mabaki ya wanadamu yakawa yako juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo hoja yangu ipo hapo kwamba mpango gani wa dharura sasa wa hiyo shida ambayo imesababishwa na ujenzi wetu itakwenda kwisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna suala la stendi ya pale ubena, mmejenga barabara imepanda juu vizuri na stendi lakini hatukuweka service road, (sehemu ya kupita waenda kwa miguu) kwa hiyo imekuwa kama kisiwa, ndiyo msingi wa swali langu kwako.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa naibu spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili analolisema tunakubali lipo, na bahati nzuri mimi hilo eneo kwa kweli nalifahamu vizuri. Nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TANROADS makao makuu, TANROADS mkoa waliokuwa wanasimamia ujenzi wa hiyo barabara ya DRT na wenzetu wa TARURA ambao sisi tuna ushoroba wetu ambao ni mdogo huko tunapokwenda kwenye makazi sisi hatutakiwi kwenda, lakini tunashirikiana na wenzetu wa TARURA kutengeneza hiyo mifereji na hasa baada ya kukamilisha huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nitumie nafasi hii kumwelekeza Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam, TANROADS Makao Makuu waweze kumshirikisha Mheshimiwa Mbunge mipango ambayo ipo na wanachokifanya ili aweze kusaidia na kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi Serikali inafanya nini ili kuondoa hiyo adha baada ya kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge watakushirikisha, watakupa mipango ya kufanya ili kuhakikisha kwamba baada ya ujenzi huu hatufanyi adha kwa wananchi ambao walikuwa na maisha ambayo hawakuwa na hayo mafuriko.
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitoe shukrani sana kwa ufafanuzi kutoka TAMISEMI juu ya kero ya michango shuleni na nina uhakika sasa, tunaenda kumaliza karaha ya michango isiyokuwa na maana ambayo mingi imekuwa inaleta lawama kwa Serikali yetu.
Mheshimiwa Spika, nilitaka nifahamu mpango wa Serikali baada ya mvua kuharibu barabara zetu huko mitaani, hasa katika Jimbo langu la Ukonga. Ni lini sasa Serikali wataanza kusambaza kifusi kwa ajili ya kujaza hizo barabara hasa za kule Ulongoni A, Ulongoni B, Barabara ya Mwembe Supu kuelekea kule Mwembe Samaki. Naomba Mheshimiwa Waziri atueleze kwamba karaha hii inakuwaje ili tuweze kuondokana na mashimo ambayo…
SPIKA: Mheshimiwa Shingo swali lako umeuliza la barabara siyo?
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, naam.
SPIKA: Swali lako ni kifusi cha barabara?
MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, kifusi kwenye barabara zetu ambazo ziko chini…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shingo kama ifuatavyo:-
Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekiri, Serikali tumetoa maelekezo mahususi kuhusiana na michango holela shuleni; lakini suala lake la barabara, kwanza nimwelekeza Meneja wa TARURA Wilaya, afike eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha na achukue hatua za dharura kuweza kusambaza vifusi hivi, ili wananchi waendelee kupata huduma stahiki. Naomba kuwasilisha.