MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja kukemea vitendo vya kutoza gharama za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inayoelekeza kutoa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum ikiwemo akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 wasio na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatangaza rasmi kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote awamu ya kwanza itakayohusisha makundi ya wananchi ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito, walemavu na wazee wasio na uwezo, ambapo kundi hili litagharamiwa na Serikali. Kukamilika kwa hatua hii kutawezesha wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kupata huduma za afya kwa kugharamiwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha kuwa wanatekeleza maelekezo ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za afya kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BAKARI B. SHINGO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kukarabati kwa dharura barabara ya Nyerere katika maeneo ya Mombasa – Gongo la Mboto na maeneo ya makaburi ya Kiltex?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bakari Bakari Shingo, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara kwa sehemu ya Mombasa hadi Gongo la Mboto kupitia mradi wa mabasi yaendeayo haraka awamu ya tatu (DRT 3). Aidha, kwa barabara ya inayopita maeneo ya makaburi ya Kiltex, tayari kuna mkandarasi anaendelea kuifanyia matengenezo kwa kuchonga tuta na kuweka tabaka la changarawe ili kuwezesha barabara kupitika majira yote ya mwaka. Kazi za matengenezo zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.