Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kassimu Amari Mbaraka (2 total)

MHE. KASSIM A. MBARAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani sana. Nina maswali mawili ya nyongeza: -

(a) Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuingia ubia na wadau mbalimbali wa michezo wenye viwanja mbalimbali ndani ya Taifa hili ili kuweza kuviendeleza, kuviimarisha na kuviboresha viwanja hivyo ili kuondoa kero na adha ya viwanja mbalimbali nchini kufungiwa mara kwa mara?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango mkakati wa kutosha ndani ya Mkoa wa Tanga tuwe na uwanja mkubwa wa kisasa wa mpira, kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haina uwanja wowote wa mpira mkubwa wa kisasa wenye kukidhi viwango na haja ndani ya Mkoa wa Tanga, ukiacha kituo kilichokuwepo cha TFF katika Kata ya Mnyanjani? Ni lini? Tuweze kupata majibu hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Amari Mbunge wa Tanga Mjini kwa maswali mazuri yenye kujenga, lakini halikadhalika kwa kuendelea kuwasemea kwa sauti kubwa wananchi wa Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishaanzisha mazungumzo na Chama cha Mapinduzi ambacho chenyewe ndicho kimekuwa na viwanja vingi katika Mikoa mbalimbali nchini, ili kuona namna ambavyo tunaweza kuingia ubia kwa utaratibu unaokubalika kwa mujibu wa sheria ili Serikali iweze kuvikarabati na kuviendesha viwanja hivi na wananchi wapenda michezo nchini wapate maeneo kwa ajili ya kufanya shughuli za michezo; iwe ni aidha kwa burudani, kwa kuweka afya zao sawa, ama kama ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mazungumzo haya hayajafa, yanaendelea na tutakapokuwa na taarifa ya nini kimefikiwa, na utaratibu gani utatumika, tutakuja kwenye Bunge lako Tukufu kuwafahamisha wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili kuhusu uwanja wa kisasa mkoani Tanga, ni kweli Serikali Awamu ya Sita chini ya mwanamichezo namba moja Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafahamu haja na hamu ya wananchi wapenda michezo kote nchini kuona kunakuwa na ongezeko pamoja na uboreshaji wa maeneo mbalimbali ya michezo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo siyo kwamba tumelifumbia macho. Kwa sasa Serikali imejielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu itakayotumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON, ambapo tunajenga uwanja mpya wa kisasa Jijini Arusha, tunafanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini tunajenga Uwanja wa Dodoma, halikadhalika na viwanja 15 vya mazoezi, pamoja na Uwanja wa Fumba kule Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapomaliza azimio hili la kuhakikisha tuna miundombinu sawasawa kwa ajili ya ku-host AFCON, tutajielekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya michezo katika mikoa mbalimbali. Serikali hivi tunavyoongea imeshaanzisha mchakato wa uanzishaji wa taasisi mahususi kwa ajili ya ujenzi na usimamizi wa miundombinu ya michezo ambayo itaitwa SIMA, na ambayo hivi karibuni pengine itakuwa tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo lake ni kuhakikisha kila mkoa na kila halmashauri nchini inakuwa na miundombinu sahihi ya michezo kwa ajili ya wananchi wapenda michezo.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa hii ndiyo reli ya kwanza kujengwa, ndani ya Taifa hili la Tanzania wakati huo ikiitwa Tanganyika. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuimarisha na kuiboresha reli ya meter gauge yaani MGR, kuweza kutoa shehena nyingi, kubwa na kutosha kutoka pale Tanga, Kilimanjaro hadi Arusha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza, je, ni upi mpango wa Serikali kukifanya sasa Kituo cha Pugu, Pugu Station kwenye reli yetu ya mwendokasi inayoenda speed ili ya express, kuweza kukifanya kuwa sasa ni kituo kama kituo kingine cha kushukia, tuseme cha tatu kutokea Dodoma na pia kutokea Dar es Salaam kiweze kutumika effectively, kwa reli ya mwendokasi inayoenda speed. Ni lini Serikali itakifanya kile kituo ni cha muhimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka kwa maswali yake ya nyongeza na nampongeza jinsi anavyofuatia maendeleo ya Mkoa wa Tanga na Kaskazini kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Serikali inasimamia Reli ya meter gauge yenye urefu wa kilometa 2,707 ambayo ilipokuwa inajengwa ufanisi wake ilikuwa ni kubeba mzigo wa takribani tani milioni tano. Kutokana na changamoto mbalimbali, reli ya Kati pamoja na Kaskazini uwezo umeshuka mpaka umefika takribani 290,000 sawa na 5.8%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari maboresho yameshaanza kwa upande wa reli ya kati na tayari ninavyozungumza Serikali imeshaagiza material kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata vitendea kazi vya kuanza ujenzi wa kutoka Ruvu kuelekea Dar es Salaam na hatua ya pili itakuwa kutoka Ruvu - Tanga mpaka Kilimanjaro, ili kuhakikisha kwamba tunaijengea uwezo kutoka kwenye speed ya ratili 20 mpaka 15 iliyopo sasa iweze kwenye uwezo wake wa 80 mpaka 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ya pili kuhusu Kituo cha Pugu ili tuweze kuongeza. Msingi wa reli ya kisasa ni kufupisha safari. Tunayo treni yetu ya kawaida inayofanya safari zake za kawaida kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma, na kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Dar es Salaam na kadhalika ambayo kutoka Dar es Salaam mpaka hapa tuna vituo karibu 10. Serikali iliamua kuweka treni nyingine ya express ambayo inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, ikitoka Morogoro kituo kinachofuatia ni hapa. Tumepokea maombi yake, lakini msingi tulidhani kwamba, tuendeleze ratiba hii kwanza, ikionekana kuna uhitaji sana baada ya uchambuzi wa kina tutafanya hivyo, kwa muda huu tunawashauri abiria wa pale Ruvu waweze kupanda treni ya kawaida ya kisasa ambayo na yenyewe inatumia masaa kama manne tu, na hii nyingine ni kama karibu masaa matatu na robo. Ahsante.