MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itafunga viti katika Uwanja wa Mpira wa Mkwakwani – Tanga kwa kuwa viti vimepelekwa na vipo uwanjani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inakipongeza Chama cha Mapinduzi pamoja na wadau wengine zikiwemo halmashauri mbalimbali na taasisi binafsi nchini kwa kuwa wadau muhimu katika kukuza na kuendeleza michezo, na hasa kwa kujenga na kutunza miundombinu mbalimbali ya michezo, hususan viwanja vya michezo ya kipaumbele; mathalan mpira wa miguu, mpira wa netiboli, mpira wa kikapu, na mpira wa wavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, viwanja hivi kikiwemo kiwanja cha Mkwakwani vimekuwa vikitumika katika kuendesha ligi kuu na mashindano mengine mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliwezesha upatikanaji wa viti 6,500 vilivyotolewa uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam wakati ukifanyiwa ukarabati, ambapo vilikabidhiwa kwa uongozi wa CCM Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kufungwa katika uwanja wa Mkwakwani. Kwa sasa uongozi wa CCM Mkoa wa Tanga umeshapata mtaalamu wa kufunga viti hivyo, na kazi inaendelea.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Bandari ya Tanga - Kilimanjaro - Arusha - Singida hadi Musoma (kilometa 1108) utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassimu Amari Mbaraka, Mbunge wa Tanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya kuunganisha reli ya Bandari ya Tanga na Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Singida hadi Musoma. Kwa sasa hatua inayoendelea ni kuhuisha yaani review tafiti hizo, ili kuendana na mahitaji ya sasa ikiwemo ushirikishwaji wa makampuni ya madini yanayowekeza kwenye ushoroba huo. Aidha, Serikali inaendelea na kufanya majadiliano na kampuni mbalimbali ili kufanya uwekezaji wa reli hii ya kimkakati.