Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hasnain Gulamabbas Dewji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kusini

Primary Question

MHE. HASNAIN G. DEWJI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa Wananchi wa Kilwa Masoko waliopisha upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege?

Supplementary Question 1

MHE. HASNAIN G. DEWJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ahadi hii ya fidia ilitamkwa na Mheshimiwa Rais Mkoani Lindi wakati amekuja kuomba kura, na ahadi ya Rais ni kama maelekezo, na kwa kuwa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo wananchi wangu walipwe fidia, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aharakishe hilo jambo kwa kuwa wananchi wangu wanateseka sana, hawana mpango wowote, huku fidia hawajapata na huku mvua zinanyesha. Kwa hiyo, ninaomba sana fidia ipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ninamwomba Naibu Waziri aje Kilwa kuona, tukae nao wanateseka sana, mvua hizi ni kubwa, hawana pa kwenda huku fidia hawajapata, huku hawajijui wanakwenda wapi? Kwa hiyo, ninamwomba sasa Naibu Waziri aje aongozane na mimi, tufuatane, aone kabla...

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Dewji kwa namna ambavyo ana-sympathize na wananchi wa Kilwa Kusini kutokana na jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza kiwanja hiki, na lazima nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yako mambo makuu matatu ambayo tunayazingatia sana katika upangaji wa bajeti. La kwanza, tunatazama Ilani ya CCM; la pili, tunatazama dira ya 2050; na la tatu, maelekezo ya viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye mwenyewe ameshasema na amekumbushia kwa niaba ya wananchi kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha dhamira ya dhati kwa kuhakikisha kwamba uwanja huu unajengwa. Pale Kilwa siyo tu uwanja, pia alionyesha dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba bandari ya uvuvi inajengwa na ninyi mnashuhudia bandari ya uvuvi sasa inakwenda kuzinduliwa. Nimhakikishie hata hili anakwenda kulifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira, Serikali kupitia Wizara yetu ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha tumeshamaliza uthamini, hatua iliyobaki ni kulipa. Tutakwenda kuharakisha kama alivyoomba ili wananchi hao wanaoteseka waweze kupata fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza kuhusiana na kuwa tayari kwenda, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, nitakuwa tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kwenye eneo kuzungumza na kuwaeleza nia dhahiri ya Serikali ili watuvumilie tunapoendelea kujipanga kwa ajili ya kulipa fidia hiyo.

Name

Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HASNAIN G. DEWJI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa Wananchi wa Kilwa Masoko waliopisha upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege?

Supplementary Question 2

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wanaozunguka Uwanja wa Ndege wa Masasi, Kata ya Mwenge Mtapika, Kijiji cha Mbonde ambao tathmini yake na uhakiki ulishakamilika tangu 2023?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, Mtwara, kwa swali lake la nyongeza juu ya wananchi wa Masasi. Ninamwomba kama ninavyowaomba na Waheshimiwa Wabunge watupe subira kidogo, kwani tumefanya tathmini viwanja takribani 14 nchi nzima na tunalipa awamu kwa awamu. Kwa kuja kwenye swali lake kulingana na upatikanaji wa fedha tutakwenda kulipa wananchi hao, watuvumilie.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HASNAIN G. DEWJI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa Wananchi wa Kilwa Masoko waliopisha upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege?

Supplementary Question 3

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa kiwanja cha ndege kilichopo maeneo ya Sanzale, Kata ya Magomeni Bagamoyo ukizingatia Mji wa Bagamoyo sasa umekuwa mji wa ikolojia ya bahari na usafiri fungamanishi? (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kufahamu ni lini Serikali inakwenda kujenga uwanja ulipo pale Bagamoyo? Ni kweli Serikali inayo dhamira ya kuujenga uwanja huo, lakini ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba uwanja huo ambao unakwenda kujengwa ni sehemu ya mradi mkubwa sana wa kiuchumi wa Bagamoyo ambao ndani yake una bandari pamoja vitu vingine vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, sasa hivi tupo kwenye mipango mbalimbali Serikalini kuhakikisha kwamba tunafanikisha, na tutakapokuwa tayari, tutakwenda kujenga uwanja huo.

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HASNAIN G. DEWJI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa Wananchi wa Kilwa Masoko waliopisha upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege?

Supplementary Question 4

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri ninatambua chini ya uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan, wananchi 737 kati ya wananchi 1,825 wameshalipwa fidia katika Kata ya Kipawa ndani ya Mtaa wa Kipunguni Mashariki kwa ajili ya wale waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa Serikali. Ni lini sasa Serikali italipa zile fidia kwa wananchi 1,088, fidia ambayo imekaa kwa muda mrefu sana? Zingatia, ni lini, Mheshimiwa Naibu Waziri?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Agnesta, Mbunge wa Segerea kwa swali lake hilo ambalo ameliuliza. Ni dhamira ya Serikali kuanzia mwaka 1967 kufanya uthamini katika uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam pale JNIA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni Rais huyu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuona wamekaa muda mrefu wananchi hawa mwaka 2022 akalekeza, tukafanya uthamini upya, ambapo ilibainika tunahitaji takribani shilingi bilioni 144, Mheshimiwa Rais ameshaanza kulipa kwa wananchi hao, takribani shilingi bilioni 66.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wananchi waliobaki 1,000 ni dhamira ya Serikali kulipa kidogo kidogo, wanakwenda kulipwa Mheshimiwa Mbunge.