Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jafari Wambura Chege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, kwa nini Serikali isiyondoe mfumo wa wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi?

Supplementary Question 1

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba zama zimebadilika, utaratibu huu wa watoto kurudi nyumbani kwenda kupata chakula, una changamoto nyingi, ikiwemo umbali wa watoto wanakoishi na maeneo ya shule yalipo, ushawishi wanaokutana nao wakati wanarudi nyumbani, na pia kuna maeneo mengine ya vijijini watoto wanaporudi nyumbani ndio wanabadilika kuwa wapishi; wanapika chakula na wanapoaliza ndipo wanarudi shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mikoa iliyobaki na utaratibu huu ni michache, je, ni kwa nini Serikali isifute utaratibu huu na kuhimiza chakula shuleni, kwa maana ya lishe, na watoto wakaendelea kupata chakula shuleni badala ya utaratibu wa zamani wa watoto kurudi nyumbani kwenda kupata chakula?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Sera na miongozo ya elimu inahimiza sana watoto kula shuleni, kwa maana ya lishe kupatikana pale pale shuleni. Hata hivyo, zoezi hili limekuwa likisuasua sana kwa sababu aidha ya elimu kwa wazazi na changamoto nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba sasa inajikita kutoa elimu kwa wazazi na maeneo mengine ili angalau jambo hili liwe shirikishi na watoto waweze kupata chakula shuleni badala ya sasa utaratibu ulivyo baadhi ya shule wanakula na maeneo mengine watoto hawapati chakula shuleni?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Jaffari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kwa kweli amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa sekta ya elimu, na tunapongeza sana wananchi wa Rorya kwa kuwa na msemaji madhubuti na imara kama Mheshimiwa Chege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunalo suala la chakula shuleni, na Serikali hii inatambua umuhimu wa wanafunzi wetu wote kupata chakula na lishe shuleni, na ndiyo maana kupitia Waraka wa Utoaji wa Chakula na Lishe wa Mwaka 2021 ukafuatiwa na Mwongozo wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Utoaji wa Chakula na Lishe Mwaka 2023. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata chakula shuleni

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa 64% ya shule zetu za msingi, wanafunzi wote wanapata chakula shuleni. 66.47% ya wanafunzi wa sekondari wanapata vyakula shuleni. Kwa hiyo, kwa wastani kuna zaidi ya kama 36% ya wanafunzi katika shule zetu za msingi na sekondari ambao mpaka sasa hawapati chakula shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi, ma-DC, Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani, Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa, tumekubaliana kwa maelekezo kwamba tutoe elimu kwa wazazi ili wazazi waone umuhimu wa kuchangia chakula kwa wanafunzi shuleni, Na wanafunzi wale ile share yao ambayo wangeipata wakiwa nyumbani, waipate wakiwa shuleni wakiendelea na masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba niitumie nafasi hii nitoe wito kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kwamba viongozi wote ngazi za mikoa, ngazi za wilaya, Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Serikali kwenye mikutano yao ya hadhara waendelee kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuchangia chakula shuleni ili watoto wetu wasome vizuri katika mazingira bora zaidi ya lishe na afya.

Name

Hemed Sumry Haidary

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, kwa nini Serikali isiyondoe mfumo wa wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi?

Supplementary Question 2

MHE. HAIDARY H. SUMRY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Mpanda inamiliki sekondari mbili za kidato cha tano na sita za Kitaifa; na huko nyuma sekondari hizi zilikuwa na magari kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanapopata dharura mbalimbali, lakini sasa hivi sekondari zote hizi hazina magari. Je, ni lini Serikali itapeleka magari kwenye shule hizi za Kitaifa ili kuwasaidia watoto wanapopata dharura? Ninakushukuru sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu za sekondari za Kitaifa kama ambazo Mheshimiwa Sumry, Mbunge wa Mpanda Mjini amezitaja, ni shule ambazo zina uhitaji wa vyombo vya usafiri. Tumeona mara kadhaa miaka miwili mitatu iliyopita Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa magari kwenye baadhi ya shule kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma za usafiri katika shule hizo zinaboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuendelea kutafuta fedha, kupata magari ili kuwezesha usafiri katika shule hizo. Tutaendelea kufanya hivyo kwa awamu ili kuhakikisha kwamba huduma za usafiri na usafirishaji katika shule zetu hizo zinaimarika. Tukifanya hivyo, tutahakikisha pia tunatoa kipaumbele katika shule za Jimbo la Mpanda Mjini.

Name

Sara Msafiri Ally

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Primary Question

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: - Je, kwa nini Serikali isiyondoe mfumo wa wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi?

Supplementary Question 3

MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Kutokana na taarifa ya hali ya ufaulu, imeonesha kwamba shule ambazo zinapata chakula shuleni wanafaulu vizuri sana ukilinganisha na shule ambazo wanafunzi hawapati chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba 52% bado hawapati chakula shuleni; kwa kuwa Serikali imetoa ada shuleni na michango mingine midogo midogo, je, Serikali haioni kwamba pamoja na maelekezo na waraka huo wa kuelekeza viongozi wa ngazi za mikoa kuhamasisha wazazi kuchangia chakula shuleni imeshindikana; na sasa kuona haja ya kuweka sheria ili watoto hawa wapate usawa katika ufaulu wa masomo yao?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Jimbo la Mvomero ni muhimu na ya msingi. Hata hivyo, ninaomba nirejee kuweka kumbukumbu sawa kwamba wanafunzi wanaopata chakula shuleni kwa ngazi ya elimu ya msingi ni 64% na ngazi ya elimu ya sekondari ni 66.47%. Maana yake ni kwamba, wastani wa 30% ndio ambao hawapati chakula shuleni, siyo 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kweli tunafahamu umuhimu wa chakula shuleni, na kweli takwimu zinaonesha wanafunzi ambao wanapata chakula shuleni wana ufaulu mzuri zaidi kwa sababu ambazo ni za wazi. Ndiyo maana Serikali imetoa mwongozo wa 2021, imetoa utekelezaji wa 2023 na tunaendelea kusimamia kupitia wazazi, viongozi wa mikoa, bodi na kamati za shule kuhamasisha wananchi kuchangia chakula kwa watoto wa shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwa na sheria, tumepokea wazo la Mheshimiwa Mbunge, tutafanya tathmini na kuona uwezekano wa kufanya utekelezaji wake.