Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwanahamis Athumani Munkunda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Chuo cha Madini Mkoa wa Shinyanga ili kujenga uwezo kwa Vijana na Wanawake katika sekta hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri, na kwa kuwa imekiri kwamba Mkoa wa Shinyanga ni mkoa wa kimkakati katika masuala ya uchimbaji ya madini, je, haioni haja sasa Serikali kuanzisha kozi maalum au taasusi maalum kwenye Chuo chetu cha VETA cha Mkoa wa Shinyanga; kama Kozi ya Teknolojia ya Maabara, Kozi ya Jiolojia ya Msingi (Basic Geographical Survey), na Kozi ya Usindikaji wa Madini (Mineral Processing), kwa kuwa kina uwezo wa kuchukua kozi hizi ili kuwarahisishia kazi wachimbaji wadogo walioko Mkoa wa Shinyanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, ni kweli kabisa Serikali imefanya kazi kubwa katika kuanzisha hivi vituo vya umahiri; center of excellence. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo cha umahiri katika eneo letu la wachimbaji wadogo pale Mwakitolyo Halmashauri ya Shinyanga?

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mwanahamisi Athumani kwa maswali yake haya mawili mazuri. Pia nitambue uzoefu wake katika sekta yetu ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi katika swali lake la kwanza la taaluma ambazo zitatolewa katika hivi vituo vya mfano, au vyuo ambavyo tumevianzisha, ni kweli katika vituo ambavyo tumevianzisha hadi sasa kama kile cha Katente, Luamgasa, na Itumbi zilizoko katika Mkoa wa Geita na Chunya, wale wachimbaji wadogo wanapewa mafunzo ya uchakataji mahiri wa madini kwa kutumia teknolojia rahisi na za kisasa pia ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuanzisha chuo chochote cha uchakataji madini au kituo cha mfano, mahitaji mahususi ya walengwa yanazingatiwa. Katika masuala geographical survey au katika utambuzi wa miamba na kila aina ya taaluma ambayo inahitajika kwa jinsi wahitaji wa kile kituo watakavyokuwa wamejipanga, yatazingatiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, vituo hivi vya umahiri ambavyo tumevianzisha nimetaja kwamba kuna cha Katente, kiko Bukombe, kuna cha Luamugasa ambacho kipo Wilaya ya Geita na Chaitumbi ambacho kiko Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki cha Mwakitolya ambacho kinakwenda kujengwa na Shirika la STAMICO ambaye ndiyo mlezi wa wachimbaji wadogo nchini, kitakapojengwa, kitazingatia maslahi na mahitaji ya wananchi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Serikali kupitia Shirika la STAMICO ni kuanza ujenzi wake katika mwaka ujao wa fedha kwa sababu hii pia ilikuwa ni ahadi ya Rais alipofanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga mwezi Disemba mwaka 2025.

Name

Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Chuo cha Madini Mkoa wa Shinyanga ili kujenga uwezo kwa Vijana na Wanawake katika sekta hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Sawa Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, wana mpango upi wa kuja kutupatia mafunzo kwa wanawake wa Mkoa wa Songwe kwa kuwa waliniahidi Bunge lililopita, lakini mpaka leo hawajatekeleza?

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake siku zote tuko tayari kwenda kutoa mafunzo kwa wadau wetu katika makundi hayo mbalimbali; wanawake, vijana, wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Mbunge amekumbushia kwamba kulikuwa na ahadi hiyo, nikimaliza kujibu maswali hapa, niko tayari nikutane naye, tupange mafunzo na tarehe ambayo tunaweza tukafanya, pengine baada ya Bunge au hata wakati Bunge likiendelea tunaweza tukawatuma wataalamu wakaendelea kutoa hayo mafunzo yanayohitajika.

Name

Sylivia Francis Sigula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANAHAMISI A. MUNKUNDA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Chuo cha Madini Mkoa wa Shinyanga ili kujenga uwezo kwa Vijana na Wanawake katika sekta hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa umeingia kwenye orodha ya mikoa yenye madini nchini, na madini ya thamani zaidi duniani yanapatikana pia Mkoa wa Rukwa. Je, Serikali imejipangaje kuwajengea uwezo wanawake wa Mkoa wa Rukwa na vijana ili waweze kuziona fursa na kuzichangamkia kabla hazijachukuliwa na wageni?

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kati ya nchi za Afrika zilizoweza kuratibu sekta ya uchimbaji mdogo, Tanzania ni kinara. Tumeweza kuwaratibu na kuwatambua katika makundi yao mbalimbali. Kuna vyama vya uchimbaji vya wanawake, vya vijana, vya wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kuwa, Mkoa wa Rukwa ndiyo unaoibukia sasa hivi kuwa mkoa wa kimadini unaojitokeza, tuko tayari kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Mama Samia, kutoa kipaumbele kuwapa elimu wanawake ambao wamejiandaa kuingia katika tasnia hiyo kwa kujipatia leseni, kwa kuunda na kusajili vikundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge awaandae wanawake wa mkoa wake, sisi tuko tayari kwenda kuwajengea uwezo.