Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Haran Nyakisa Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Primary Question

MHE. HARAN N. SANGA aliuliza: - Je, lini wafanyakazi wa Tanzania watapunguziwa riba ya mikopo na kufikia asilimia saba au nane?

Supplementary Question 1

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze tu majibu ya Serikali, lakini nataka kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zetu zinazoitwa commercial banks zinategemea vitu viwili katika kufanya biashara, kwa kutumia consumers’ loan na Government Bond, kwa sababu hivi vitu vyote vina security kwao. Kwa Serikali kuacha watumishi ambao wamekuwa wakitumikia miaka yao 55, 60 mpaka 65, amekuwa akifanya kazi za Serikali, kwa sababu tunaamini kabisa watumishi wa Serikali siyo wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mshahara wake ndicho kitu pekee ambacho anakitegemea ili aweze kupata mkopo aweze kujenga nyumba, apate mkopo aweze kutengeneza maisha yake ya kujikimu kwa ajili ya kustaafu. Je, Serikali ina kauli gani ambayo itawasaidia watumishi hawa kuanza kuwa-motivate katika kufanya kazi, na pia kuwasaidia kwamba watapokuwa wanastaafu, wawe na maisha bora ya kujikimu?

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Sanga, anauliza maswali haya bila shaka ni kutokana na kwamba wafanyakazi hawa ni dada zetu, ni kaka zetu na wengine ni wanetu. Kwa hiyo, maisha yao na matumaini yao ya kuishi kwa kufanya kazi, mwisho wa siku yawe na faida kwao. Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi ya kifedha kwa watumishi kama ambavyo imekuwa ikifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliunda mfuko maalum wa Advances Fund kupitia Tangazo la Serikali Na. 709 lililotoka mwaka 2018 likisomeka kama “Advances Fund Establishment Order.” Lengo kuu la kuanzishwa mfuko huu ilikuwa ni kuwezesha utoaji wa mikopo kwa watumishi wa umma kwa masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Advances Fund huwa inatozwa kwa gharama ya jumla ya asilimia nne, ambayo kimsingi huwa ni kwa ajili ya services charges na bima tu ya huo mfuko. Mpango huu unawahusisha wafanyakazi au tuseme watumishi wa umma, kwa maana ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na utekelezaji wa utaratibu huu, Serikali ilielekeza taasisi nyingine za umma kuanzisha mifuko yao ya ndani ya utoaji mikopo kwa watumishi wao kwa lengo la kuhakikisha wanapata mikopo yenye masharti nafuu na hivyo kuwezesha kuimarisha ustawi wa uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2021 hadi Januari, 2026 watumishi hao wamekopeshwa zaidi ya shilingi bilioni 497, lakini kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 pekee watumishi wamekopeshwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 74.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, watumishi hao wataendelea kuishi kwa matumaini na watastaafu wakiwa wanawezeshwa na Serikali, na bila shaka mpango huu utaendelea kufanyika na jitihada nyingine za kuwezesha wafanyakazi waweze kuwa na maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)