Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yannick Ikayo Ndoinyo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Primary Question
MHE. YANNICK I. NDOINYO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo ya malisho kutoka hekta milioni 3 mpaka 6 kama Ilani ya CCM inavyosema?
Supplementary Question 1
MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sekta hii ya ufugaji inaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi, je, Serikali inaweza kuchukua hatua zipi za dharura kuwaandaa wafugaji kabla na wakati wa nyakati za ukame ili wasipoteze mifugo yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ni mikakati gani Wizara inaichukua kuwatembelea na kuwaandaa wadau pamoja na wafugaji kujiandaa na hiyo mikakati ya miaka mitano mnayoipanga kama Wizara?
Name
Ng'wasi Damas Kamani
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro, kwani tangu ameapishwa hapa mbele ya Bunge lako Tukufu amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana changamoto mbalimbali zinazowakumba wafugaji wake.
Mheshimiwa Spika, nikijielekeza katika kujibu maswali yake mawili ya nyongeza; moja linalohusika na hatua za dharura ambazo tunazichukua kuwaandaa wafugaji wetu. Kwanza kabisa ni kuendelea kutoa taarifa kupitia vyombo vyetu habari ambavyo vimekuwa vikitoa taarifa kila siku juu ya mabadiliko ya tabianchi na mipango ya hali ya hewa inavyoendelea.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili, kulingana na mipango ambayo tunayo kwa wafugaji wetu kwa kipindi hiki cha miaka mitano, ni kweli, Serikali inatambua kwamba nchi yetu ya Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, zimekuwa zikikumbwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta ukame ambao kwa kiasi kikubwa umeathiri wafugaji wetu. Kwa kulitambua hilo, sisi kama Serikali, tumechukua hatua zifuatazo: -
Mheshimiwa Spika, moja, ni pamoja na miradi mikubwa ya ujenzi wa mabwawa tunayoendelea nayo katika sehemu mbalimbali nchi nzima. Pia tunatambua kwamba miradi hii inachukua muda na fedha nyingi, hivyo tumekuja na mipango ya dharura. Kwanza, kuanza kufanya tathmini kwa ajili ya kuanza kujenga visima virefu katika maeneo mbalimbali ya wafugaji wetu.
Mheshimiwa Spika, pili, tumeendelea kufanya mazungumzo na Wizara ya Kilimo ambayo kwa kiasi kikubwa inayo bajeti kubwa kupitia Tume yake ya Umwagiliaji ambayo inajenga mabwawa ya kumwagilia kwenye sekta ya kilimo sehemu mbalimbali nchi nzima ili kupitia mabwawa hayo, basi na wafugaji wetu waweze kutengenezewa majosho kwa ajili ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Spika, pili, Wizara yetu kwa kutambua changamoto ya malisho tuliyonayo, tumeendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kupata majani ya malisho ya wanyama wetu. Majani haya tumeyafanyia tafiti, ni majani ambayo yanalimwa kwa kiasi kidogo na kupata mavuno mengi ambayo yanaweza kulisha wanyama wetu kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, tatu, pamoja na kuendeleza mashamba yetu yaliyo katika sehemu mbalimbali nchi nzima ikiwepo Shamba letu la Vikuge lililopo Pwani, lakini Shamba letu la Lagwira lililopo Mbeya na taasisi zetu mbalimbali kama TARI na LITA zinazozalisha malisho.
Mheshimiwa Spika, pia, tumeendelea kuhamasisha sekta binafsi na wafugaji wetu kuendelea kulima malisho mbalimbali. Kupitia hili, Serikali yetu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeshatenga fedha, shilingi milioni 223 ambazo tutakwenda kuanzisha mashamba darasa ya malisho ya mifugo 300 nchi nzima katika halmashauri zote ili wafugaji wetu pale wanapohitaji mbegu, basi ziwafikie kwa ukaribu na kwa wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, kwa maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha wafugaji wetu wanapata malisho haya kwa wepesi alituelekeza sisi tupunguze bei ya malisho haya ambayo tulikuwa tunauza hapo awali kwa shilingi 4,000 kwa kilo na kwa sasa kwa maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Rais, wafugaji wetu watapata malisho haya (mbegu hizi za malisho) kwa shilingi 1,000 tu kwa kilo ili waweze kuyapata kwa wepesi.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa tunaendelea kuwahamasisha wafugaji wetu…
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ameshakuelewa ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved