Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selina Henry Kingalame

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SELINA H. KINGALAME aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mfumo wa Elimu ya Vitendo (Internship) kwa kada nyingine za elimu, kama ilivyo Elimu ya Utabibu?

Supplementary Question 1

MHE. SELINA H. KINGALAME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, nini kauli ya Serikali kuhakikisha hizi internships zinaanza kutolewa kwa haraka kwa kada zote za kitaaluma, ili kuondoa ombwe la wahitimu wengi kukosa fursa za ajira kwa kigezo cha uzoefu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa, changamoto ya uzoefu imekuwa kilio cha muda mrefu, je, Serikali haioni haja sasa hizi internships ziwe ndiyo uzoefu hitajika kwa wahitimu wanapoomba ajira, na siyo miaka miwili, mitatu na kuendelea? Ahsante. (Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, Serikali inatambua umuhimu wa kuanzisha na kuimarisha Mfumo wa Mafunzo kwa Vitendo katika kada mbalimbali ili kuwawezesha vijana kupata uzoefu unaohitajika. Serikali itaendelea kufanya tathmini kuhusu upanuzi wa utoaji wa mafunzo kwa vitendo katika kada nyingi tofauti zaidi ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa endelevu na wenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, Serikali inatambua kuwa, kigezo cha uzoefu kwa wahitimu katika baadhi ya nafasi ni kikwazo. Ndiyo maana tumeendelea kufanya tathmini juu ya upanuzi wa mafunzo haya kwa vitendo ili kuona kwamba mafunzo haya yanakuwa sehemu ya kuwatayarisha wahitimu kuingia katika soko la ajira. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako na kutoa maelezo, ninaomba na mimi nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniona na kunipa heshima hii ya kuwa Waziri ninayesimamia eneo la utawala bora na utumishi wa Umma ndani ya ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, ninaomba kwanza kumpongeza Naibu Waziri kwa maelezo mazuri aliyoyatoa, ambayo ni ya ukweli pasi na shaka kwamba, ndiyo utaratibu Serikali imeweka, lakini liko jambo moja la kuongeza katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024, kwa maana ya mwaka wa kifedha 2024/2025, Serikali ilikamilisha mwongozo wa kujitolea. Mwongozo ambao unatakiwa sasa uende kwa wadau ukajadiliwe ili uweze kuwa na input ambazo kila mmoja atakuwa nazo, lakini kila kada ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge katika maswali yao, nayo itakuwa imeangaliwa ili kuweza kujibu masuala na matakwa wanayotaka wananchi wa Tanzania juu ya mfumo mzima wa kujitolea ili kufanya elimu ya vitendo iweze kuwa na ubora unaotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kitabu hicho au mwongozo huo tutaupitisha katika vikao vinavyohusika kupitia Kamati za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, utaletwa katika Bunge lako ili baada ya Bunge kuidhinisha, basi mfumo huo sasa utangazwe rasmi uweze kwenda kuwa mfano katika elimu ya kujitolea na vitendo itakayokwenda kuzaa matunda mazuri kwa kesho ya Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)