Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Revocatus Chipando Clayton
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia wakandarasi wanaochelewesha miradi kama Mradi wa Delta ya Mto Luiche unaoendelea kwa kasi ndogo?
Supplementary Question 1
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu kutoka kwa Naibu Waziri wa Kilimo, mimi ninasikitishwa sana na hiki kinachoendelea katika huu mradi wa Bonde la Mto Luiche.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zimekopwa Kuwait tangu mwaka 2018. Ukienda pale mpaka leo hii ninavyoongea na wewe, anavyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mradi umeanza, wako wanafyagia miaka nane. Miaka nane tangu tumekopa fedha mpaka leo hii wako wanafyagia tu, wanasema wanakusanya vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kama itampendeza, twende wote akajionee vituko vinavyoendelea pale katika Bonde la Mto Luiche. Fedha tumekopa, tumechukua Kuwait, tena fedha hizi alizipambania Mheshimiwa Zitto Kwabwe, alikuwa ndio Mbunge. Mheshimiwa Zitto kamaliza muda wake, mradi haujatekelezwa, kaja Mheshimiwa Ng’enda Kilumbe...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, uliza swali la nyongeza.
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza, ninaomba Serikali, tufunge nayo safari kwenda kwenye Bonde la Mto Luiche wakaone kwa macho waache maneno ya kuhadithiwa. Twende naye Naibu Waziri aende pale akaone kwa macho yake nini kinachoendelea pale katika Bonde la Mto Luiche. Hilo ndilo ombi langu. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Baba Levo, Mbunge wa Kigoma Mjini kwa concern yake, na sisi kama Wizara tunaelewa hayo anayoyaeleza. Jambo moja tu nimthibitishie, tutaenda kabla hili Bunge halijaisha, tutaongozana, tutakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutapanga moja ya weekend tutafika eneo la mradi, lakini kwa kifupi tu nieleze kwamba, kwa nini mradi huo umechelewa? Hayo anayoyaeleza ni kwamba changamoto ilikuwa ni upatikanaji wa fedha na ndiyo maana Tume ya Umwagiliaji mwaka 2025 ilifanya mapitio upya ya huu mradi, na sasa hivi mradi huu tunautekeleza sisi wenyewe kupitia fedha za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa ni kwamba kuna kama shilingi bilioni 8.89 ambazo tutazitoa kwa mkandarasi kama sehemu ya malipo mengine ya awali ili kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kwa wakati. Matarajio yetu kabla mwaka 2030 mradi huu utakuwa umekamilika na Baba Levo atawaeleza wananchi kwamba moja ya jitihada zake kubwa alizozifanya Bungeni ni kuhakikisha mradi huu umekamilika kwa vitendo. (Makofi)
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia wakandarasi wanaochelewesha miradi kama Mradi wa Delta ya Mto Luiche unaoendelea kwa kasi ndogo?
Supplementary Question 2
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kuishukuru Serikali kwa kunipatia shilingi 1,800,000,000/= kwa ajili ya kuboresha umwagiliaji Kata ya Miamba. Hata hivyo, katika fedha zile, aliwekwa mkandarasi, akafanya kazi ambayo badala ya kuboresha mifereji ya Kata ya Miamba, sasa hivi mifereji ile imerudi kwenye asilimia sifuri ya utekelezaji, wakati fedha hizo zilitoa uwezo wa mifereji kufikia 70%.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kwamba fedha za Serikali shilingi bilioni 1.8 alizopewa mkandarasi hazikufanya kazi yoyote kwenye umwagiliaji Kata ya Miamba na Mkakimbili ya Kata ya Miamba sasa hivi? Ahsante.
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninamshukuru mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki kwa swali la msingi hususan katika kata yake ya Miamba Tarafa ya Mambavunta nafikiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali tulitoa hiyo fedha, na kwa sababu tumepokea changamoto hii, naomba nimwelekeze Meneja wa Mkoa wa Umwagiliaji afike katika hilo eneo atupe taarifa ya tathmini; lakini mimi mwenyewe nilishaahidi mara ya kwanza na narudia tena, nitafika katika eneo hilo ili sasa moja, tuone thamani ya fedha iliyotumika, na pia tuchukue hatua stahiki kama haya ambayo ninaamini Mheshimiwa Mbunge anayasema hayajatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi Serikali ambao tunamsaidia Mheshimiwa Rais, hatutakuwa tayari kuona wananchi wanashindwa kuhudumiwa ipasavyo. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved