Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Ngonyani Msongozi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mshangano – Legele hadi Mletele?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana katika kuchagiza uchumi katika Manispaa ya Songea. Wanawake wamekuwa wakipata adha kubwa kupeleka bidhaa zao masokoni.

(a) Je, Serikali ni lini itaanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

(b) Serikali imeeleza hapo kwamba inatakiwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kilometa tano. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha na vifaa vya ujenzi, graders, caterpillars ili ujenzi huu uanze mara moja kwa ajili ya kuchagiza uchumi katika Manispaa ya Songea? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi za Wilaya, barabara zinazosimamiwa na TARURA hasa kwa maana barabara hizi zinachangia sana katika shughuli za uchumi na kuwawezesha wananchi kufika katika huduma za msingi kabisa za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona katika Wilaya ya Songea, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya shilingi bilioni 20 zimetumika katika kuimarisha miundombinu ya barabara hizi za Wilaya. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, shilingi bilioni 7.65 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumjibu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi kwamba lini ujenzi wa barabara hii utaanza, kama nilivyotangulia kusema, tayari usanifu umefanyika katika barabara hii ya Mshangano – Legele, na imebainika kwamba shilingi bilioni 2.5 zinahitajika kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kilometa tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa, fedha itakapopatikana, ujenzi utaanza, ataona wakandarasi wako site, ataona hiyo mitambo anayotaka kuiona, ataiona ipo site, kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii, kwa sababu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana kiuchumi, lakini inawasidia wananchi kufikia huduma za msingi za kijamii.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mshangano – Legele hadi Mletele?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga barabara ya Mtandika – Ikula, Kata ya Ruaha Wilaya ya Kilolo? Hii barabara nimepita mimi Jumapili, haipitiki. Mimi mwenyewe nimekwenda kwa bodaboda tu, hata bodaboda zinapita kwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu moja ambayo inatakiwa itengenezewe mawe ili mwamba uweze kutoka. Wananchi wanapata mateso makubwa sana hasa akina mama wajawazito kwenda kwenye kituo cha afya. Ni mateso makubwa sana.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwamba Serikali inaendelea na inafanya uwekezaji mkubwa sana katika eneo la kuimarisha barabara zetu hizi za Wilaya zinazosimamiwa na TARURA. Barabara hii ya Mtandika anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ambayo ipo Kilolo, Serikali itafika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa ili iweze kuwanufaisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuendelea kumsisitiza Meneja wa TARURA wa Mkoa pamoja na Meneja wa TARURA wa Wilaya waendelee kufanya tathmini na kubaini barabara muhimu za msingi kabisa kama hizi ambazo zinahitaji uwekezaji wa Serikali, kwa maana ya kuziimarisha barabara hizi ili sasa fedha iweze kutengwa, iwe kwenye mipango na bajeti kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kumhakikishie Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwamba Serikali itafika kwa ajili ya kuja kuhakikisha barabara hii inajengwa ili iweze kuwanufaisha wananchi wa Kilolo. (Makofi)

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mshangano – Legele hadi Mletele?

Supplementary Question 3

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru pia Naibu Waziri kwa majibu mazuri na ya uhakika anayotupatia, na watu wanasubiri utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, katika Awamu ya Tano wakati wa kampeni, wananchi wa Uru katika Kata ya Uru Magharibi, eneo la Uru Shimbwe waliahidiwa kwamba barabara yao itatengenezwa kuanzia Rau – Uru Shimbwe Kwa Kinyasha, wakati wa kuweka jiwe la msingi Awamu hii ya Sita pia waliahidiwa jambo hilo hilo. Kwa hiyo, viongozi wawili wa juu waliahidi. Je, ni lini sasa barabara hiyo ya Rau – Shimbwe Kwa Kinyasha itajengwa?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake, inaweka kipaumbele kikubwa sana kwa ahadi za Viongozi Wakuu. Mheshimiwa Shally Raymond ametoa historia kidogo kueleza kuhusiana na ahadi ya ujenzi wa barabara hii ya Rau – Shimbwe. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Shally Raymond kwamba Serikali tayari imeiweka barabara hii katika mipango yake kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inakuja kuijenga ili iweze kuwanufaisha wananchi katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kutoa kauli ya Serikali kwamba Serikali itakuja kuhakikisha inatekeleza ahadi hii muhimu kabisa iliyotolewa na viongozi wetu ili wananchi waweze kupata barabara nzuri ambayo itawasaidia katika majukumu yao, kwa maana ya shughuli za kiuchumi, na pia kufikia huduma za msingi za kijamii.