Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zaytun Seif Swai
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka unakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninashukuru kwa majibu ya Serikali. Mradi huu wa Magadi Soda wa Engaruka ni moja kati miradi ya kimkakati na ni mradi muhimu sana kwa ajili ya kutuongezea ajira pamoja na fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, wawekezaji wengi wanavutiwa kuwekeza kwenye mradi huu lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa miundombinu sahihi inayoelekea kwenye mradi; Barabara ya Selela – Engaruka ni mbovu sana lakini hakuna maji wala umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha Wizara hizi zinasomana ili miundombinu hii iweze kujengwa kwa haraka? Ahsante.
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, kwanza, ninachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Zaytun Swai kwa kuendelea kufuatilia mradi huu muhimu sana. Kama alivyosema mwenyewe, kweli ni wa kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutekeleza hii miradi ya kimkakati kama ambavyo alianza kwenye ule Mradi wa Liganga na Mchuchuma na sasa tunaenda kutekeleza Mradi huu wa Magadi Soda kwa sababu mradi huu unasaidia ukuaji wa viwanda vingi na utekelezaji wa mkakati ule mkubwa unganishi wa Maendeleo na Viwanda (Integrated Industrial Development Strategy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mkakati huu mkubwa, moja ya mradi ni huu wa Magadi Soda. Kama nilivyosema, tumeshaanza kwanza kulipa fidia na kutoa elimu kwa wananchi ili kupisha mradi. Zaidi sasa nimesema kwenye jibu langu la msingi, tunachoenda kufanya sasa ni kuanza kuweka bajeti ya kuweka miundombinu wenzeshi ikiwemo hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaja; barabara, maji, umeme na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mradi huu ili utekelezwe ni lazima haya yote yakamilike. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake na nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaenda kutekeleza mradi huu kama ambavyo tumeanza kutekeleza miradi mingine ili isaidie kupunguza uagizaji wa bidhaa au malighafi hii ambayo inatumika kwenye viwanda vingi ikiwemo viwanda vya vioo, sabuni, rangi, karatasi, kusafisha mafuta ya petroli na kadhalika, ambayo tunatumia fedha nyingi sana za kigeni kuagiza kutoka nje wakati tunayo hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved