Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2020-2025 | Session 19 | Sitting 53 | Works, Transport and Communication | Wizara ya Ujenzi | 688 | 2025-06-25 |
Name
Dr. Paulina Daniel Nahato
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuongeza fedha za mkopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wenye mahitaji maalumu?
Name
Omari Juma Kipanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Answer
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Daktari, ninaomba nichukue nafasi hii kipekee kabisa kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, na kuwashukuru Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge lako hili Tukufu kwa malezi yenu katika kipindi chote cha miaka mitano. Ushauri wenu kwa Serikali, maoni na miongozo yenu ambayo mara kwa mara mmekuwa mkitupatia sisi kama Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa upande wa Wizara ya Elimu, hili ni swali letu la mwisho kwenye Bunge hili, na niwaombee heri Wabunge wote tuje kuonana tena hapa mwezi wa Kumi na Moja tukiwa na afya njema, Mwenyezi Mungu akatuvushe huko tunakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, sasa ninaomba kujibu swali la Dkt. Nahato, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu mwaka hadi mwaka ili kuwawezesha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu ambao ni wahitaji na wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi ili kuwawezesha kumudu gharama za masomo ya Elimu ya Juu na kufikia ndoto zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za mikopo zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 787 mwaka 2024/2025 na idadi ya wanufaika imeongezeka pia kutoka wanafunzi 145,000 mwaka 2020/2021 hadi 235,799 mwaka 2024/2025 wakiwemo wenye mahitaji maalumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, utoaji mikopo unawapa ahueni wanafunzi wenye mahitaji maalumu au wenye wazazi wenye ulemavu kwa kuwapatia kipaumbele katika upangaji wa mikopo ili kuwawezesha kumudu mazingira ya chuo katika kipindi cha masomo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya wanafunzi 2,398 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2024/2025 kupitia kigezo cha mahitaji maalumu. Serikali inaendelea kupokea ushauri na maoni ya wadau kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau ili kubainisha aina ya uhitaji unaostahili kupewa kipaumbele bila kuathiri dhana ya uhitaji inayotamkwa na sheria. Ninakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved