Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 29 Education, Science,Technology and Vocational Training, Maswali kwa Waziri Mkuu 4 2026-05-14

Name

Latifa Khamis Juwakali

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, unafahamu kwamba ada za wanafunzi wa vyuo vikuu ni muhimu sana kwa kuendesha vyuo vyetu, lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya vyuo vikuu kuwazuia wanafunzi ambao hawajamaliza au hawajakamilisha ada kufanya mitihani mwishoni mwa mitihani.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ataungana nami kwamba baadhi ya wananchi ambao hawajakamilisha ada hizo ni kwa sababu pengine ni kutokana na umaskini wa wazazi wao au kukosa ada au kukosa ada ya mikopo ambayo ni matarajio makubwa ya vijana ya nchi hii. Ni ipi kauli ya Serikali ili kuwapa moyo vijana vya nchi hii? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Latifa Juwakali, kwa kuwasemea vyema vijana wetu wa Kitanzania hasa wanatokea familia za kawaida za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upo utaratibu ambao ni wa pande zote kwamba ada zile zinasaidia hivi vyuo au taasisi ziweze kujiendesha hasa zile ambazo hazipokei ruzuku ya Serikali kwa kiwango cha kuweza kujiendesha. Hata hivyo, upo kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba inatokea katika baadhi ya wanafunzi wanakwama kabisa kutokana na mazingira alikotokea.

Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu ambao umekuwa ukitumika miaka mingi hata enzi ambapo hapakuwa na elimu bila ada ilikuwa ni wanafunzi kuruhusiwa kufanya mitihani, lakini watakapotakiwa kuchukua vyeti vyao, watalazimika kulipa kwanza zile ada ambazo hawakuwa wamezilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nielekeze taasisi zetu za elimu kuzingatia utaratibu ule ambao umekuwa ukitumika wa kutokuwazuia wanafunzi kufanya mitihani, kwa sababu mitihani ni jambo la maandalizi. Mwanafunzi anakuwa ameshajiandaa, yuko tayari kwa ajili ya mitihani, na jambo la ada siyo la kwake. Kwa hiyo, anapata adhabu kutokana na hali halisi ya kimaisha ya familia yake. Hili ni jambo ambalo siyo jema.

Mheshimiwa Spika, turejee kwenye ule utaratibu ambao mitihani ikifika, wanafunzi wafanye mitihani, wapimwe, kwa sababu hawapimwi kwa ada, wanapimwa kwa maandalizi ya mafunzo waliyoyapata na utaratibu ule wa kwamba atakapohitaji cheti chake lazima awe amemaliza mahitaji yote ya kimalipo ambayo alitakiwa kuyafanya.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, taasisi ziendelee kuwa-engage kuongea na wazazi mara kwa mara kuwakumbushia kwamba kuna mahitaji ya kifedha ambayo mwanafunzi wao, ama mtoto wao hajayamalizia ili waweze kuweka utaratibu wa kuyalipa bila kuathiri masomo ya mwanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anayelipa ada anakuwa mzazi, siyo mwanafunzi. Kwa hiyo, mwanafunzi jukumu lake ni kusoma, na vyuo pamoja na kuzingatia ukweli ule kwamba vinatakiwa kupata fedha ili viweze kujiendesha, utaratibu mzuri zaidi ufanyike ule ambao uliendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza fedha kwenye upande wa mikopo ya elimu ya juu na vyuo vya kati ili kuongeza idadi kubwa zaidi ya watoto ambao wananufaika na mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, fedha zinazokwenda kwenye mikopo ya elimu ya juu zimeongezeka kwa takribani mara mbili kutoka shilingi bilioni takribani 400 hadi shilingi bilioni 900 na ziada, jambo ambalo tunaamini limeongeza pia idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai pia kwa wanufaika ambao waliwahi kunufaika na mikopo kuendelea kurejesha ili Serikali iweze kuwapatia wanafunzi wengi zaidi wigo wa kupata mikopo hiyo na kunufaika na elimu ya juu.

Additional Question(s) to Prime Minister