Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 29 Natural Resources and Tourism Maswali kwa Waziri Mkuu 3 2026-05-14

Name

Thomas Maganga Kampala

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Primary Question

MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi nchini inayohusisha wananchi na hifadhi za misitu. Migogoro hii inapelekea migongano ya mara kwa mara kati ya TAWA, TFS na wananchi, jambo ambalo husababisha vifo vya wananchi na kuchomewa mazao yao.

Mheshimiwa Spika, mfano mdogo ni kwenye Jimbo langu la Katavi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja akatoa maelekezo, lakini maelekezo yale hayajazingatiwa. Hivi tunavyoongea, kuna sintofahamu, wananchi wanachomewa mazao yao na wanazuiwa kuvuna. Nini kauli ya Serikali kwenye jambo hili? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Thomas Kampala kwa kulileta jambo hili. Ni kweli kumekuwepo na migogoro kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyoitaja, imedumu kwa muda mrefu. Hata katika ziara ukiondoa jambo la migogoro ya ardhi ya mtu na mtu, mtu na taasisi, eneo lingine linalofuatia ni migogoro hii inayohusisha watu pamoja na taasisi zetu za uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwanza, kama nchi, ni lazima tukubaliane kwamba kila mtu anatakiwa aheshimu sheria; wananchi pamoja na watekeleza sheria. La pili, imekuwa kukitokea matatizo ya kiusimamizi kwamba watu wanaachwa wanalima kama ni mazao, wanalima. Wakishamaliza kulima ndio unakwenda utekelezaji wa sheria, ikihusisha kuwazuia kuvuna na kufyeka mazao. Hilo jambo siyo la kiungwana na halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nielekeze, maeneo yote ambako hatukuchukua hatua ya kuzuia, hatukuchukua hatua ya kutoa elimu; ikiwa wananchi wameshakamilisha kulima, wako kwenye hatua za kuvuna, tusifanye kazi ya fyeka mazao yao wala tusifanye kazi ya kuvuna kwa niaba yao. Waacheni wavune, lakini tukishamaliza kuvuna maeneo yote yale ambayo tunajua hayapaswi kulimwa, maeneo yote ambayo tunajua hayapaswi kufungwa, hutumia kwa mifugo, tupeleke elimu ya kuwaelezea wakulima wasilime katika msimu wa kilimo utakaofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo hilo, zipo tuhuma pia kwamba baadhi ya wasimamia sheria wanaacha makusudi watu walime halafu wao wakachukue yale mazao. Katika baadhi ya maeneo wanaenda kuyafyeka tu ya yule ambaye hajaweza kuwapa fedha katika baadhi ya maeneo, wanaacha wale ambao wanatoa fedha walime ilhali wale ambao hawajatoa fedha wanawafyekea. Hivyo hivyo na masuala ya kiufugaji, wapo ambao makundi mengine ambao wanaona wameweza kuelewana kwa namna yoyote ile, wanawaacha na wale ambao hawafikii makubaliano, wanawanyang’anya mifugo yao. Double standard ya aina hiyo haikubaliki.

Mheshimiwa Spika, sasa nitumie jukwaa hili kuelekeza kwamba maeneo ambayo wakulima walishalima, wasifyekewe mazao yao. Baada ya mavuno, ifanyike kazi ya kuwaelekeza maeneo ambayo hayapaswi kulima, maeneo ambayo hayapaswi kufugia ili tuweze kwenda na kuheshimu sheria na kuweza kuheshimu maeneo yale ambayo tumekubaliana yatumike kwa matumizi maalum.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, hata kunyang’anya vyombo. Nilipita eneo moja nikakuta wamenyang’anya trekta la mtu mmojawapo ilhali wengine mashamba yao yapo. Kwa hiyo, inaonekana tu lengo ilikuwa ni lile trekta.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mashamba, wapo waliolima, hii na yenyewe haikubaliki. Nilisema matrekta ya aina hiyo yarudishwe kwa wahusika ili tuanzie pale mwanzo, tutoe elimu na tuzuie watu kwenda kufanya shughuli za uzalizaji kwenye maeneo ambayo yamezuiwa.

Additional Question(s) to Prime Minister