Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 29 | Works and Transport | Maswali kwa Waziri Mkuu | 2 | 2026-05-14 |
Name
Isack Joseph Copriano
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, unajua fika mwaka huu nchi yetu imepata mvua nyingi za kutosha na kusababisha barabara nyingi kukatika na kukosa mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka fedha za dharura wakati tukisubiri bajeti ya 2026/2027 kutekelezwa ili kurudisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika?
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Isack Joseph almaarufu Kadogoo, kwa swali zuri ambalo linagusa maeneo mengi ya nchi yetu. Ni kweli kumetokea uharibifu katika maeneo mbalimbali ya barabara zetu zote zinazohudumiwa na TANROADS na zile zinazohudumiwa na TARURA.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua madhara hayo ambayo yamejitokeza kutokana mvua zilizonyesha maeneo mengine zikiwa ni mvua nyingi kuliko ilivyotarajiwa. Hata hivyo, pamoja na tathmini hiyo kufanyika, kama unavyojua, masuala ya kiujenzi huwa yanategemea pia hali ya hewa kwamba huwezi ukafanya ujenzi imara ikiwa mvua zinaendelea. Kwa hiyo, Serikali inachofanya, imechukua hatua za dharura maeneo ambako mafuriko yalisababisha kukosekana kwa mawasiliano, kurejesha mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ujenzi wa kurejesha miundombinu katika hali ya kawaida unatarajiwa ufanyike baada ya mvua kupungua. Kwa utaratibu huo, uwezekano mkubwa wa ujenzi huo utaanza kufanyika tutakapokuwa tumeshaanza kutekeleza bajeti mpya ya Serikali. Katika utekelezaji wa bajeti hiyo mpya ya Serikali Wizara zetu hizi; Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI zinazosimamia TARURA na TANROADS wana mafungu ya matengenezo ya barabara mpya, pia wana mafungu ya kufanya matengenezo ya kurejesha barabara ambazo zilikuwa zimeharibika.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaweka mkazo, na mahitaji ni takribani shilingi bilioni tatu kwa upande wa barabara za TARURA na zaidi ya shilingi bilioni nane kwa upande wa barabara zinazohudumiwa na TANROADS. Serikali itaweka nguvu kuhakikisha tunarejesha barabara hizo zirejee katika hali yake ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, maelekezo ya Mheshimiwa Rais, ambayo ndiyo maelekezo ya Serikali, ni Wizara zetu hizi na taasisi zetu zinazojenga barabara, kuhamia kwenye ujenzi wa kutumia teknolojia ya kisasa na kujenga barabara za kudumu hasa katika maeneo korofi ili kuepusha uwezekano wa kuwa kila mwaka tunapeleka fedha, halafu mvua ikinyesha mara moja au mara mbili, ile fedha yote inazolewa na mafuriko.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaelekeza pia kwenye kujenga barabara zinazodumu hasa kwenye maeneo korofi ili kuepusha hasara ambayo inajitokeza ya kila mvua inaponyesha fedha hizo zinakwenda na maji. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved