Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 24 Energy and Minerals Maswali kwa Waziri Mkuu 5 2026-05-07

Name

Janeth Elias Mahawanga

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha hivi karibuni, dunia imekumbwa na changamoto ya kisiasa na kiuchumi ukiwemo migogoro ya Kimataifa ambayo imeleta changamoto ya upatikanaji wa mafuta katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania. Hali hii imeleta sintofahamu na athari kubwa za kupanda kwa maisha na gharama za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali imechukua hatua gani katika kukabiliana na athari hizi za migogoro ya kidunia na Kimataifa zinazopelekea changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu swali zuri la Mheshimiwa Janeth Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kufuatia mambo yanayotokea Mashariki ya Kati, kumekuwepo na madhara hasi kwenye uchumi, na siyo tu kwa Tanzania, ni kwa dunia nzima, nchi zote duniani, zinapata madhara haya; nchi zilizopo kwenye eneo la mapigano, nchi zinazoshiriki kwenye mapigano, na nchi nyingine zote, ikiwemo Tanzania ambayo ina sera yake ya kutokufungamana na upande wowote.

Mheshimiwa Spika, katika madhara hayo, kumekuwepo na kupanda kwa masuala ya bei za mafuta, kupanda kwa gharama za bima, kupanda kwa mnyororo mzima wa distribution, mgawanyo wa ugavi, na pia kumekuwepo na mashaka ya uwezekano wa kuadimika kwa bidhaa zenyewe katika nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua kama nilivyowahi kusema, na Mheshimiwa Waziri wa kisekta amewahi kuisemea pia katika sehemu mbalimbali ya maelezo. Ni kwamba Serikali kwanza imefanya tathmini ya kina kujua ukubwa wa tatizo, madhara ambayo yanajitokeza katika sekta zetu za kiuchumi; na pili, hatua ambazo zinafaa kuchukuliwa ili kuweza kuhakikisha kwamba madhara haya hayawi makubwa zaidi pamoja na kwamba ni kweli madhara yatakuwepo na Tanzania siyo kisiwa.

Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza ambayo Serikali imechukua ni ya kuhakikisha kwamba bidhaa hii haiadimiki. Zipo nchi ambazo tayari matatizo yameshajitokeza ya bidhaa hiyo kuadimika, kwamba hata kama una fedha hupati mafuta.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mkakati kuhakikisha la kwanza bidhaa hii ya mafuta haiadimiki; na pili, Serikali imechukua hatua ya kufanya masuala ya ruzuku ambayo tayari kuna taratibu za namna ya kutekeleza zoezi hilo la ruzuku, ambapo zimekuwepo njia nyingi ambazo zinatumika kwa ajili ya kuweza kuhakikisha tunapunguza makali ya madhara yanayotokana na kile kinachoendelea kule Mashariki ya Kati.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, tunatumia uzoefu tuliofanya jambo la aina hii lilipotokea pale palipokuwepo na mzozo kule Ulaya Mashariki. Lilitokea jambo lililoleta madhara kama haya, na Serikali iliendelea kutoa ruzuku kwa namna mbalimbali za ruzuku ili kuhakikisha kwamba bei hazipandi hasa kwa nishati hiyo ambayo ni injini ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, mbali na hilo, pia Serikali imekaa na wadau, imewasikiliza. Mimi pamoja na Mawaziri wa sekta tulikaa na wadau, wakiwemo wadau wa usafirishaji ili kuweza kujadiliana nao na kuhakikisha tunadhibiti kupanda kwa gharama za usafirishaji ambapo zikipanda gharama hizo kimsingi itakuwa inaashiria pia kupanda kwa gharama za maisha.

Mheshimiwa Spika, tulikubaliana na wasafirishaji kupunguza gharama ambazo wanazipata katika baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali, ambazo kimsingi siyo za lazima sana na haziathiri sana mambo ya Serikali ili ikiwa ni namna ya kutoa ruzuku kwamba tukiwapunguzia gharama hizo, wao watatumia hiyo fedha ambayo walikuwa wanalipia katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanatolewa maelekezo na Serikali, itumike kupunguza bei za gharama za usafiri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kulikuwepo utaratibu wa mabasi yote yanapokwenda mikoani, lazima yapite kila stendi hata kama hayana abiria wa kushusha. Tumesema hakuna ulazima wa kila basi kupita kila stendi hata kama halina abiria wa kushusha ili kuweza kupunguza gharama kwa mabasi haya na gharama hizo zilizopunguzwa, zitumike kama ruzuku ya kutokupandisha bei.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, pia kuna mabasi ambayo yameshatengenezwa ambayo hayana uwezo wa kubeba mzigo mkubwa zaidi ku-overloads, kuliko uwezo wake wa jinsi ilivyotengenezwa. Mabasi haya pia kila wakati yalikuwa yanapita kwenye vituo vyetu vya kupima uzito, kwenye weigh bridge zetu, yalikuwa yanapita hata kama muundo wa basi lake hauruhusu kubeba mizigo mikubwa iliyopitiliza, wanapanga foleni ndefu, wanachoma mafuta, wanaingia gharama.

Mheshimiwa Spika, tumesema mabasi hayo ambayo kwa utengenezaji wake hayawezi yakabeba mzigo mkubwa kuliko ambayo umekadiriwa, hayana ulazima wa kupita kwenye mizani, yenyewe yatapitiliza moja kwa moja ili kupunguza gharama ya kuchoma mafuta na kupandisha gharama kwa wasafirishaji.

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, hata yale ambayo yanatakiwa kupima uzito, tumepunguza vituo vya kupita kupima. Watapita sasa kwenye mizani ya kwanza na ya mwisho kabla hawajamaliza safari yao walikokuwa wanaenda.

Mheshimiwa Spika, hizi zote ni njia mbalimbali za utoaji wa ruzuku, kupunguza gharama ambazo zingeweza kubebwa na mwananchi kwa maana ya madhara ambayo yatakuwa yamejitokeza kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya tathmini na kuchukua hatua ili kuweza kuhakikisha bidhaa hii haiadimiki, lakini pia kuhakikisha inaendelea kuwa affordable, na himilivu, bei ambazo Mtanzania anaweza akamudu na kuendelea kusukuma uchumi kwa nchi yetu.

Additional Question(s) to Prime Minister