Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 24 Health and Social Welfare Maswali kwa Waziri Mkuu 4 2026-05-07

Name

Bonnah Ladislaus Kamoli

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Primary Question

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kauli ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba wapendwa wetu wanapokuwa wamepeleka wagonjwa wao na bahati mbaya wameondokewa na wapendwa wao, basi hospitali zetu za Serikali ziweze kuachia hiyo miili, lakini bado kuna sintofahamu katika hospitali nyingi kuendelea kushikilia ile miili kwa kuwaomba hawa watu waweze kutoa fedha ili waweze kuachiwa miili ya wapendwa wao. Je, ni ipi kauli ya Serikali?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nijibu swali zuri la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwepo na utamaduni ambao ulijengeka miaka mingi wa kuzuia miili ya wapendwa wetu pale inapokuwa imetokea bahati mbaya amefariki, kwa ajili ya kubishania kuhusu masuala ya kulipia gharama za matibabu zilizofanyika.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi wakati wa kampeni, na waraka ukatolewa na mpaka sasa tunasimamia utekelezaji wake kwamba inapotokea bahati mbaya kama hiyo, fedha isiwe kigezo cha kushikilia mwili wa mpendwa wetu anapokuwa ameshatutoka, hasa tukitambua kwamba kuna baadhi ya imani zetu haziruhusu kukaa na mwili muda mrefu kabla ya kuupumzisha.

Mheshimiwa Spika, kwa swali hili, na kwa maelekezo yale ya Mheshimiwa Rais, nisisitize tena kwenye hospitali zote za umma kuhakikisha kwamba wanatekeleza maelekezo haya, na watekeleze mwongozo ambao umetolewa wa namna ya kutekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni rahisi tu. Imetokea, mpendwa wetu ametutoka, tunazo kumbukumbu, masuala yote ya kitabibu yamekamilika, waruhusiwe mara moja kuchukua mwili. Kumbukumbu zao zinajulikana, mambo ya bill yajadiliwe wakishamaliza suala la kumsindikiza mpendwa wao.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai tu kwa Watanzania wote kwamba jambo hili limekuwa likijitokeza kwa sababu ni kweli huwa tuna taratibu za masuala ya uchangiaji wa matibabu. Uchangiaji wenyewe unafuata taratibu hizo ambazo zimeorodheshwa. Unapokwenda hospitalini kuna masuala ya vipimo, kuna masuala ya dawa, pamoja na mambo mengine yanayohusiana na matibabu.
Mheshimiwa Spika, jambo hili, Mheshimiwa Rais amekuja na jawabu la kudumu, ambalo ni Bima ya Afya kwa Wote. Kwa Watanzania wote tupokee dhana hii, tupokee sera hii, tupokee jambo hili na sote tujiunge kwenye suala hili la Bima ya Afya kwa Wote ili tuweze kumaliza kabisa tatizo hili la kudaiana bili, hali ukiwa umeshaondokewa na mpendwa wako.

Mheshimiwa Spika, tukishakuwa na Bima ya Afya kwa Wote, maana yake, masuala haya ya matibabu yatakuwa sasa yanaendeshwa kwa taratibu za bima, ambapo hakutakuwepo na mambo ya kulipialipia kila hatua unapokwenda pale hospitalini. Inakuwa unapata matibabu kwa kutumia utaratibu wa bima ambao ndiyo utaratibu ambao umeonesha mafanikio katika maeneo mengi hapa duniani.

Additional Question(s) to Prime Minister