Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 24 | Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives | Maswali kwa Waziri Mkuu | 3 | 2026-05-07 |
Name
Rebeca Sanga Nsemwa
Gender
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali. Kwa kuwa, wanawake wengi Tanzania wanaojihusisha na shughuli za kilimo wanapatikana vijijini na wanatumia zana duni za kilimo, je, ni lini Serikali itawasaidia wanawake hawa kwa kuwaunganisha na benki za kilimo ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu na hatimaye waweze kufanya kilimo cha kisasa, chenye tija na kisha Serikali iwasaidie kutafuta masoko ya mazao yao ndani na nje ya nchi? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi niweze kujibu swali zuri la Mheshimiwa Rebeca Nsemwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika maeneo mengi yanayojihusisha na kilimo, moja ya wahusika wakuu katika shughuli hiyo ya kilimo ni wanawake na wamekuwa nguzo katika familia nyingi hapa nchini. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza, Serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha na taasisi za kifedha na pengine taasisi za kifedha zisogee karibu na kule walipo?
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na inakubaliana na ushauri na wazo zuri lililotolewa na Mheshimiwa Mbunge. Kwa sasa Serikali imekuwa inatumia Benki yetu ya Kilimo, TADB, pamoja na taasisi nyingine za kifedha, ambapo Serikali imetengeneza majukwaa ya kuwaunganisha wakulima, hasa akina mama, waweze kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu ambayo itawawezesha kutekeleza shughuli hiyo vizuri. Taasisi nyingine ambazo zimefanya kazi hiyo ni pamoja na wenzetu wa PAS, Benki kama ya CRDB, NMB na TCB.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, Serikali pia, imefanya marejeo kuangalia uwezekano wa mikopo ile inayotolewa ngazi za Halmashauri, kuruhusu wigo wa matumizi yake. Kwa yule ambaye anataka aitumie katika shughuli za kilimo, kwenye ile 4% ambayo inaangukia upande wa wanawake, aweze kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania iko hatua za mwisho pia kukamilisha kampuni ambayo itakuwa inasimamia kutoa dhamana, ambapo kwa zamani ilikuwa chini ya dirisha lile la Export Credit Guarantee Scheme. Sasa kuwe na kampuni, ambayo itakuwa na madirisha mbalimbali ya kuweza kusaidia makundi mbalimbali, likiwemo kundi la wanawake, kundi la vijana, kundi la vijana wasomi kutoka vyuo vikuu waweze kupata dhamana kupitia kampuni ambayo itakuwa inadhamini mikopo ili makundi hayo ya akina mama ama vijana yaweze kupata mikopo katika taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea, tayari tuna shilingi bilioni 280 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kwenda kutekeleza jambo hilo. Kwa hiyo, ni jambo ambalo litakamilisha taratibu za kisheria ili kuweza kuhakikisha mwamba linaanza kufanya kazi zake na akina mama waweze kupata mikopo hiyo.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved