Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 24 | Health and Social Welfare | Maswali kwa Waziri Mkuu | 2 | 2026-05-07 |
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nchini Tanzania kumeibuka watu ambao hatuna hakika kama ni wataalamu, wanatoa elimu ya namna ya ulaji. Utasikia anasema, ili kupunguza kitambi kula hivi, kula hivi, bila kumjua yule anayempa ushauri ana uzito kiasi gani, ana urefu kiasi gani au anafanya shughuli gani? Kwa hiyo, wimbi limekuwa kubwa na wananchi wakati mwingine wanachanganyikiwa na hizi theory za ulaji.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali sasa ina mpango gani wa ku-centralize utoaji wa elimu kwa watu mahususi wenye taaluma hiyo ili kuondoa mkanganyiko ulioko kwenye jamii yetu sasa? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Ninatumia fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumetokea wimbi kubwa la watoa elimu ya masuala ya lishe na afya. Hii ni kutokana na kukua kwa uelewa, pengine wa masuala ya afya. Kwa sasa tuna wataalamu wengi wanaojua masuala ya afya kutokana na kupanuka kwa elimu ya masuala ya afya kutoka kwenye vyuo vyetu. Kwa sasa ni kweli, wigo wa vyuo vyetu umeongezeka sana.
Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kumeongezeka wimbi hilo la kutoa elimu kwa sababu njia za kutoa elimu zimeongezeka. Zamani ilikuwa chombo cha habari rasmi, itakuwa ni TV au ni redio, ambayo ni rasmi. Sasa hivi kila mwananchi anaweza akatoa ujumbe wake pale pale alipo kupitia mitandao ya kijamii. Kwa hiyo, huu ni wigo mwingine ulioongezeka tofauti na zamani, ambapo kulikuwa na madarasa rasmi, TV rasmi na redio rasmi ya Taifa. Sasa kuna njia hii ya mitandao ya kijamii ambako kuna majukwaa mengi, kuna kurasa nyingi ambazo mtu anaweza akatoa elimu yake.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, swali aliloleta Mheshimiwa Saashisha ni la msingi na ni jambo ambalo linatokea. Serikali itaendelea kusimamia sera, sheria, pamoja na miongozo inayohusu afya na masuala ya lishe, ili kuweza kulinda usalama. Kwanza, usahihi wa elimu inayotolewa, na pili, usalama wa wananchi wetu kufuatia kile ambacho kinatolewa kwenye mwongozo huo.
Mheshimiwa Spika, ninatambua tuna Sheria ya Afya, tuna Sera ya Afya, tuna Sera ya Masuala ya Lishe na tuna Miongozo, ambayo inasimamia masuala hayo ya lishe. Mbali na hilo, taaluma ya masuala ya kiafya inatawaliwa pia na mabaraza yanayozisimamia. Ninatumia fursa hii kuwaelekeza wenzetu wa Wizara ya Afya, pamoja na Mabaraza yale yanayosimamia Tasnia hizo za Taaluma ya Afya kuendelea kuzingatia, huku tukifanya tathmini kuhusu uwezekano wa kuratibu masuala ya leseni na vibali kuhusu watoa elimu hiyo ya afya na lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge ninaweza nikatolea mfano kidogo. Zamani Wanyiramba walikuwa wanataniwa kwamba ni watu wanaokula punda. Najua ulikuwa ni utani, na kama ni kula, ni kuonja kidogo. Ikaja ikatokea kwenye hawa watoa elimu waliokuja, sijui ni yupi, akasema kwamba, nyama ya punda inaepusha ugonjwa wa gout kwenye magoti.
Mheshimiwa Spika, ghafla tukasikia mnada wa nyama ya punda umejengwa kule kwa wenzetu Wanyaturu, Damankia. Hatujakaa sawa, tukasikia na Wairaq kule Manyara wanatafuta mnada wa nyama ya punda. Hatujakaa sawa, tukasikia Warangi huku Kondoa wanatafuta mnada wa nyama ya punda, na siyo ajabu ukakuta hata kwa Wagogo kuna mnada wa punda. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, la msingi ninalotaka kusisitiza ni kwamba hatuna uhakika kama kweli kile kilichosemwa kwamba ukila nyama ya punda inaepusha ama inatibu gout. Hatuna huo uhakika, lakini ndiyo hivyo, yule aliyetoa taarifa ile ameshawachongea punda wetu. Sasahivi ukitafuta punda kule ni shida kuwapata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo aliloleta Mheshimiwa Mbunge, tutazingatia kusimamia miongozo ili taarifa inayotolewa iwe ni ya kweli na imethibitishwa kwamba ni ya kweli, na hakuna madhara kwa kile kilichoshauriwa. Ninakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved