Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 24 Lands, Housing and Human Settlement Development Maswali kwa Waziri Mkuu 1 2026-05-07

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Gender

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mwuliza swali namba moja kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya, kwa ajili ya kupeleka tabasamu kwa wananchi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua dhamira njema ya Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi, hasa kupitia ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati nchini, ikiwemo barabara, bandari, viwanda na viwanja vya ndege. Katika kufanikisha miradi hiyo, Serikali imekuwa ikitwaa maeneo mbalimbali kutoka kwa wananchi ili kufanikisha maendeleo haya. Baadhi ya maeneo ambayo Serikali imeyatwaa yapo Kipunguni, Jimbo ya Segerea, Kilwa, Mwanza Chato, Nachingwea na kwingineko.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya wananchi hawajalipwa fidia kwa miaka mingi sana na jambo hili limesababisha adha kubwa sana, ambapo wananchi wanashindwa kuendelea na maisha yao mengine.

Mheshimiwa Spika, ni ipi kauli ya Serikali katika kutatua kero hii, kwa kuwalipa fidia zao wananchi hawa, ili hatimaye nao waweze kuendelea na maisha mengine ikizingatiwa kwamba, hawajiendelezi katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushuru kwa kunipa nafasi hii niweze kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert. Ni kweli, kumekuwepo na utwaaji wa maeneo kwa ajili ya kutimiza malengo mapana ya Kitaifa kwa masilahi mapana ya Taifa letu, hasa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, jambo la kutwaa maeneo lipo kisheria. Kwa mujibu wa sheria yetu inayoongoza utwaaji wa maeneo, mwananchi anawajibika kuachia maeneo yake ya ardhi ili kuwezesha nchi kutekeleza miradi yenye masilahi mapana ya Kitaifa. Hata hivyo, sheria inayoongoza utwaaji wa maeneo inaelekeza kwamba, mwananchi mwenye eneo lake la ardhi analolimiliki kwa hati, ama umiliki wa asili, anapopisha miradi ya maendeleo anapaswa kulipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, swali alilolileta Mheshimiwa Mbunge ni la msingi, na ametaja moja ya eneo la Kipunguni na maeneo mengine, kama alivyoyataja. Imetokea kwa muda mrefu takribani miaka 15 mpaka 20 hivi iliyopita, yamefanyika makosa hayo ya kutwaa maeneo bila kulipa fidia, ambapo yamelimbikiza mzigo mkubwa wa ulipaji wa fidia hizo, hasa maeneo ambayo tayari yamechukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inachofanya, na kauli ya Serikali ni kwamba, Serikali itaendelea kuheshimu Sheria hiyo ya Utwaaji wa Maeneo kwa kulipa fidia kwa kila mwananchi, ambaye ameachia eneo lake la umiliki lenye hati, ama umiliki wa asili, kwa ajili ya kupisha mradi wa maendeleo wenye maslahi mapana kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka yake minne, mitano ya mwanzo amelipa fidia maeneo mengi sana ambayo yametwaliwa zamani, ikiwemo kule Liganga, Mchuchuma; ikiwemo kule Engaruka na maeneo ya viwanja vya ndege. Hata hili la Kipunguni, deni lilikuwa kubwa sana, ninavyokumbuka litakuwa limelipwa linaelekea halfway. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kuna hao wananchi wengine ambao Mheshimiwa Mbunge ameuliza. Ninakumbuka nimewahi kufika pale Kipunguni nikiwa Waziri wa Fedha, nikiwa nimetumwa na Mheshimiwa Rais, kwenda kujionea hali halisi, lakini pia, kuweza kuanza kutekeleza njia ya malipo, na imefanyika kwa kiwango kikubwa, lakini bado kuna sehemu ambayo haijalipwa. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kulipa fidia za maeneo ambayo Serikali imeyatwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utwaaji wa maeneo mengine umekuwa siyo tu kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na hapo ndipo ambapo tatizo linapoanzia. Yapo maeneo ambayo yamechukuliwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini bila kufuata utaratibu huu. Yapo maeneo ambayo nimepita hata kwenye ziara nimejionea, lakini yapo maeneo mengine ambayo siyo hata kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, inatokea pana mwananchi anamiliki eneo kihalali na hati anayo, anatokea mwananchi mwingine analitafuta eneo hilo kwa misingi ya uwekezaji ama biashara, anatuma viongozi wa Serikali kwamba, nichukulieni lile eneo ili niweze kutekeleza mradi na inaenda kutumika Sheria ile ya Utwaaji wa Maeneo kwa masilahi mapana ya Taifa. Hilo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mwananchi ana miliki eneo lake kihalali na ana hati, siyo uungwana na siyo utaratibu wa kisheria kulitwaa bure ili umpe mwingine ambaye amelitamani eneo hilo. Kama umetamani eneo la mwananchi mwenzako na una shughuli nalo, nenda na fedha, lipia eneo ili na yeye aweze kuendelea na maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukianzisha Kliniki ya Ardhi hapa, utakuta hata Wabunge, wapo ambao maeneo yao yametwaliwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli nyingine na fidia bado haijalipwa. Sasa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba, mwananchi asinyang’anywe ardhi yake anayoimiliki kwa sababu yoyote ile. Lazima alipwe fidia ili na yeye aweze kubadilisha maisha yake, aweze kupata utajiri kupitia urithi huo alionao ambao wengi wa Watanzania urithi wao ni ardhi. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister