Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 3 | Regional Administration and Local Government Authorities | Maswali kwa Waziri Mkuu | 6 | 2026-04-02 |
Name
Bahati Keneth Ndingo
Gender
Female
Party
CCM
Constituent
Mbarali
Primary Question
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Tunatambua kwa mujibu wa mitaala yetu ya elimu iliyopo nchini na utekelezaji wake, mwakani mwaka 2027 watoto wetu wa Darasa la Sita na la Saba wote watakwenda kufanya mtihani wa kuhitimu masomo yao ya shule ya msingi na hivyo tutakuwa na mzigo mkubwa sana wa kuanza kidato cha kwanza. Idadi itakuwa mara mbili ya ile ambayo imezoeleka.
Mheshimiwa Spika, kwa kulingana na miundombinu iliyopo na mikakati ya kibajeti iliyopo, je, Serikali ina uwezo na mikakati gani ambayo imejiwekea kuhakikisha kwamba watoto wetu wote watakwenda kuanza kidato cha kwanza? Ninakushukuru sana. (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri kweli. Yeye ni mama, anawaza kuhusu watoto kuanza masomo, na wote waanze masomo bila kuathiriwa na utekelezaji wa mitaala mipya.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha swali kinachosema je, Serikali imejidhatiti na ina uwezo wa kutekeleza jambo hilo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndiyo. Serikali imejipanga kwa jambo hilo, imejidhatiti na hatuna mashaka kwamba tutatekeleza kikamilifu jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Serikali ya Awamu ya Sita, awamu ya kwanza ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alijenga madarasa takribani 79,000, alijenga shule za msingi zaidi ya 2,700, na alijenga shule za sekondari zaidi 1,300. Hiyo inatupa confidence, itatupa kujiamini kwamba hata hili la kwenda kuanza kutekeleza mitaala mipya litawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tathmini imeshafanyika na kila kona nilikopita nimewaelekeza Wakuu wa Mikoa pamoja na timu zote za Serikali za Mitaa kufanya tathmini na kufanya maoteo ya mahitaji haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema.
Mheshimiwa Spika, jana nilisema hapa kwamba tulikuwa tukiongelea kuwa na sekondari kila kata, lakini kwa sasa tunapoongelea kuwa na elimu ya lazima mpaka kidato cha nne, kimsingi tunaongelea kuwa na sekondari kila Kijiji. Kwa maana hiyo, tutakuwa na uhitaji wa nyongeza ya madarasa matatu kwa kila kijiji ili kuchukua yale saba yaliyokuwepo, tuongeze matatu, ili tuwe na madarasa 10. Katika baadhi ya maeneo watoto ni wengi huenda uhitaji wa madarasa ukawa mkubwa kuliko huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa tathmini ya haraka tutahitaji takribani madarasa mapya zaidi ya elfu ishrini na tatu kama na mia mbili hivi na tutakuwa tunahitaji maabara mpya zaidi ya elfu tisa kama na mia tatu hivi. Tayari tulishafanya maoteo ya rasilimali ambapo patahitajika takribani trilioni moja na sehemu hivi kwa ajili ya kutekeleza programu hiyo.
Mheshimiwa Spika, tumeotea pia idadi ya wanafunzi, kwa kuwa kwa sasa waliokuwa wanajiunga na kidato cha kwanza ilikuwa takribani 900,000 kwenda 1,000,000, lakini kwa uhitaji huo wa madarasa mawili kuanza kwa mara moja kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tutakuwa na watoto wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza takribani 3,000,000 hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna nyongeza ya kama 2,000,000 kwenye idadi ambayo tulikuwa tukiipokea kwa kila mwaka. Kwa hiyo, tumekadiria haya mahitaji ya rasilimali na tayari hata sasa tumeanza kujenga shule za aina hiyo ambazo zinafuata muundo huo.
Mheshimiwa Spika, hata nilipokuwa Katavi nilikagua shule mojawapo ambayo ina shule ya msingi pale pale na shule ya sekondari pale pale ambapo shule za aina hiyo tayari zimeshajengwa kama 6,000 hivi ambazo zinaunganisha katika compound moja shule ya msingi na sekondari pale pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kujenga zile nyingine zinazopungua huku tukitambua kwenye makao makuu ya kata tulipokuwa na shule za sekondari za kata, maana yake tayari tutakuwa na shule za msingi ambayo iko pale pale kwenye kijiji ambacho ni makao makuu ya kata, lakini tuna sekondari ambayo ilikuwepo pale pale.
Mheshimiwa Spika, ambapo tuna sekondari takribani 5,000 ukiondoa zile ambazo zina kidato cha sita huenda tukawa na sekondari kwenye 3,000 kwenda 4,000 ambazo ziko kwenye makao makuu ya kata. Kwa hiyo, hizo na zenyewe zitatufanya kuwa na madarasa ambayo yanaweza, kwa mpito yakatekeleza mkakati huu kwamba tuna sekondari pale na tuna shule ya msingi katika kijiji husika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika maeneo ambayo sasa hatuna shule za sekondari, tutalazimika kuongeza madarasa matatu matatu ili kuweza kukidhi uhitaji wa madarasa hayo pamoja na maabara.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais anatambua pia kwamba shule siyo madarasa tu, na shule siyo maabara tu, na shule siyo madawati tu, ndiyo maana pia Mheshimiwa Rais ameendelea kutoa vibali vya ajira, na ndani ya siku 100 za uongozi wake tayari walimu 7,000 wameshaajiriwa na kupelekwa katika vituo vya kazi na vibali vingine vilivyatoka ambapo kazi hiyo itaendelea kuhakikisha kwamba tunaenda sambamba na miundombinu, pia na walimu wa kuwafundisha watoto. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved