Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 3 | Information, Culture, Arts and Sports | Maswali kwa Waziri Mkuu | 4 | 2026-04-02 |
Name
Abdul Yussuf Maalim
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Amani
Primary Question
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa AFCON ya pamoja mwaka 2027. Sambamba na maandalizi hayo, kutahitajika miundombinu bora ya upatikanaji wa huduma za kijamii zinazokubalika katika viwango vya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa viongozi wetu wamehakikisha ujenzi wa viwanja vya kisasa vinawajumuisha Marais wetu; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia, pale Arusha pamoja na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi pale Fumba, Zanzibar. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wajasiriamali wetu wananufaika na mashindano hayo? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri na ufuatiliaji alioufanya kuhusu fursa zinazoweza kujitokeza kufuatia kwa Tanzania kuwa mwenyeji kwenye mashindano makubwa ya Barani Afrika ya AFCON.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya AFCON. Ndani ya Serikali tumeshaanza kukaa vikao mbalimbali. Mbali na vile vya maandalizi, tunakaa vikao ambavyo vinajadiliana kuhusu ni namna gani Tanzania itanufaika na kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa Barani Afrika.
Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo tumeyabainisha yatakuwa na faida ya moja kwa moja ni yale yanayowahusisha wafanyabiashara wadogo wadogo ambapo katika viwanja vyote ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano na vile ambavyo vitatumika kwa ajili ya mazoezi, vitakuwa na mazingira ambayo yatawawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kuweza kunufaika na ujio wa wageni hawa ambao watashiriki katika mashindano.
Mheshimiwa Spika, tunatarajia pia katika maeneo hayo ya viwanja vya mazoezi, ya viwanja vya mashindano barabara zake ziwe na taa ili kuwezesha wafanyabiashara wa hizi biashara ndogo ndogo kufanya biashara majira yote. Pia, kuwepo na matoleo ya namna ambavyo biashara hizo zinaweza zikafanyika katika maeneo hayo kwa njia ambayo wageni hawatalazimika kwenda kuzitafuta maeneo ya mbali. Kwa mfano, tuna vitu vya asili, tuna vitu vya vivutio, vitu vya kitamaduni, kuna vitu vinavyoweza kupatikana kwa uharaka ambavyo vinatengenezwa ndani ya nchi na vitu vingine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara zinazohusika tayari wameshaanza kuandaa mikakati hiyo ikiwemo Wizara inayohusika na mambo ya biashara, mambo ya vijana, mambo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara nyingine kama Maendeleo ya Jamii ambazo moja kwa moja zitakuwa na makundi ambayo yanaweza yakawa na bidhaa ambazo zitawaingizia kipato kwa kuuza kwa wageni watakaohusika, watakaoshiriki katika mashindano hayo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved