Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 3 Industries and Trade Maswali kwa Waziri Mkuu 2 2026-04-02

Name

Ado Shaibu Ado

Gender

Male

Party

ACT

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kuniona. Vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeleta madhara makubwa sana kwa uchumi wa dunia. Ukiacha suala la kupanda kwa bei ya mafuta ambalo umeshalitolea mwongozo jana, wachambuzi wa mambo wanasema kwamba vita hii ina matokeo makubwa sana yenye athari hasi kwenye biashara ya Kimataifa katika sekta ya bima, sekta ya uagizaji wa bidhaa muhimu, biashara ya madini, na usafiri wa anga wa Kimataifa. Hii maana yake ni kwamba Tanzania haipo salama.

Mheshimiwa Spika, swali kwa Waziri Mkuu, ninataka kujua ni kwa namna gani Serikali imefanya tathmini juu ya athari ya vita hivi kwa mipango ya kiuchumi ambayo tunaendeleanayo na mingine tutakayoipanga hivi sasa na hatua ambazo imejipanga kuzichukua? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mfuatiliaji wa masuala yanayoendelea duniani. Ni kweli vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati na vilivyotangulia huko Ulaya ya Mashariki ni tatizo kwa dunia nzima. Kutakuwa na madhara kwa dunia nzima na Tanzania siyo kisiwa, ni nchi ambayo inategemeana; inafanya biashara, inafanya mawasiliano, na pia ina ushirikiano na nchi zote duniani.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya tathmini ya awali kupitia sectors mbalimbali ndiyo maana tumeweza kupata maoteo kwamba kutakuwepo na mabadiliko ya bei katika baadhi ya shughuli zetu za kiuchumi, ikiwemo la awali kabisa ambalo limeshajitokeza la kupanda kwa mafuta, lakini na mengine kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge aliyoyataja yakiwemo ya bima.

Mheshimiwa Spika, kutakuwepo pia na matatizo yatakayojitokeza yanayohusiana na matatizo kwenye masoko ya fedha kule duniani ambapo sekta binafsi na Serikali tumekuwa tukitumia kama chanzo cha kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa njia mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali katika kukabiliana na hilo, moja, tunajua tutahitaji zaidi kama ambavyo Mheshimiwa Rais alishatoa kauli, tutahitaji zaidi kutumia rasilimali za ndani katika kuhakikisha tunatekeleza miradi ya maendeleo ili shughuli za miradi ya maendeleo ziendelee na nchi iendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika, katika baadhi ya maeneo ambayo tunatarajia kuendelea kuyaboresha kama ambavyo nilisema na kwenye hotuba tutaweka nguvu kubwa katika kutafiti kwenye madini, tuongeze uchimbaji na mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha uliopita, moja ya sekta iliyotuletea mapato mengi ilikuwa ni madini. Utaona kwamba ongezeko hilo halijatokana tu na migodi mikubwa, limetokana na wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzania ambao wameongezeka katika shughuli za uchimbaji na wameongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, hata mwaka 2025 kwenye makadirio ya Wizara walitakiwa wakusanye takribani zaidi ya shilingi trilioni 1.2. Kwa miezi hii tu kabla mwaka wa fedha haujaisha, tayari walishakusanya takribani shilingi trilioni moja. Unaweza ukaona kwamba hiyo ni sekta ambayo ni rasilimali zilizo ndani ya nchi yetu ambayo inaweza ikafanyika kama chanzo cha mapato kama tutaongeza wigo.

Mheshimiwa Spika, unakumbuka utafiti ambao ulishawahi kufanyika ni 16% tu. Kwa hiyo, bado tunayo fursa, nchi yetu kila wilaya ni madini. Kwa hiyo, hii ni moja ya sekta ambayo tunadhani tutaongeza nguvu ya utafiti ili tuweze kujitegemea kimapato ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine tunalotarajia kulifanyia kazi ni kubana matumizi. Lazima tubane matumizi katika maeneo ambayo siyo ya lazima ili kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo, hii ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na hali ya dunia ambayo italeta mtikisiko katika masuala ya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, tutafanya tathmini ya kina kwa sababu jambo hili halijakadiriwa exactly madhara yake yataisha lini, na jambo lenyewe litaisha lini? Kwa hiyo, tutafanya tathmini ya kina, na kwa sababu Bunge lako linaendelea, tutaendelea kujulishana kuhusu hatua zipi nyingine ambazo Serikali inatarajia kuzichukua ili kuweza kukabiliana na jambo la aina hii.

Additional Question(s) to Prime Minister