Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kijakazi Mohamed Yunus (2 total)

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba kufahamu wananchi wa Kata ya Nanjirinji Wilayani Kilwa Mkoani Lindi wamekuwa wakipata adha ya kuvuka Mto Mbwemkuru kuelekea Wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya kufuata huduma za dharura. Daraja hili lilisombwa na masika mwaka 2024. Sasa nataka kufahamu, je, ni lini Serikali itajenga daraja hili ili kuwaondolea wananchi hawa adha hususan wanawake wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, na bahati nzuri hilo daraja nilipita kabla na hata baada ya kusombwa. Ni barabara ambayo inaunganisha Ruagwa – Nanjirinji hadi Kiranjeranje.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ule mpango wa kujenga madaraja ya dharura, kulikuwa na madaraja matatu katika hiyo barabara. Moja, ni hilo Mbwemkuru ambayo ni daraja kubwa, mto mkubwa, na pia tuna Daraja Nakiu na Kigombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakiu na Kigombo yamekamilika. Hili daraja la Mbwemkuru liko kwenye mpango wa kujengwa na mfadhili wa World Bank kwenye kuratibu mradi unaoitwa CRW; inavyosema, mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kuanza kulijenga hilo daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni taratibu tu, zikikamilika na wenzetu wa World Bank, daraja hilo linaweza kujengwa ili kuondoa hiyo adha, ahsante.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa barabara iliyoelezwa hapa, Barabara ya Ngongo – Milola – Michiga kwa muda mrefu sana imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Pamoja na jitihada za Serikali za kufanya marekebisho mara kwa mara, ningependa kufahamu, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ukizingatia kwamba barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Jimbo la Lindi Mjini, Mchinga na Jimbo la Ruangwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi kuwa kama alivyosema, barabara hii inaunganisha majimbo mawili; Jimbo la Mheshimiwa Salma na Mheshimiwa Mmuya. Wamekuwa pia wakifuatilia sana kuhusu ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Tumekwishafanyia usanifu na sasa tunatafuta fedha tuijenge kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kati ya barabara zetu ambazo sasa hivi tunatafuta teknolojia mpya ambayo ni rahisi kujenga barabara kwa kiwango cha lami. Hii ni moja ya barabara ambayo ipo kwenye mpango wa kuifanyia pia majaribio katika hiyo teknolojia mpya. Kwa hiyo, tuna uhakika wakati tunatafuta fedha, lakini pia imeingia kwenye mpango wa kufanyia majaribio, hii tunayosema teknolojia mpya ya barabara.