MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED aliuliza: -
Je, lini Mkataba wa kuchakata Gesi Asilia (LNG) Lindi utasainiwa na kuanza utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Kijakazi Yunus Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali na wawekezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia (LNG) Mkoani Lindi wapo katika hatua ya mwisho ya majadiliano, hususan kwenye masuala ya kisheria ili kuwezesha usainishaji wa mikataba na makubaliano, na hatimaye utekelezaji wa mradi kuanza. Aidha, wabia wa mradi wameendelea na miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Mpya ya Likong’o ambayo ujenzi wake umefikia 90%.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko sambamba na kuwalipa fidia wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kijakazi Yunus Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha zoezi la uthamini wa mali za wananchi wanaopaswa kupisha utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko. Kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi husika kwa kuzingatia miongozo na taratibu za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapenda kusisitiza kuwa ulipaji wa fidia ni hatua ya msingi kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hiyo. Hivyo, baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Serikali itaanza taratibu za maandalizi ya utekelezaji wa mradi, ikiwemo upatikanaji wa fedha za ujenzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa upanuzi wa kiwanja unatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga.