Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninaungana na wachangiaji waliopita kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha sisi sote kuwa wazima wa afya na kukutana hapa kwenye Bunge Tukufu siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali na kuweza kusimama hapa mbele ya Bunge hili Tukufu na kuweza kuzungumza machache kwa niaba ya Wanawake na wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii pia kuungana na waliotangulia kuchangia, kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninapenda kumwita malkia wa nguvu. Mheshimiwa Rais kama wengine walivyoeleza, amefanya kazi kubwa sana ya kuliletea maendeleo Taifa letu na sisi wanawake wa Mkoa wa Lindi na wananchi wa Lindi kwa ujumla tumekuwa sehemu ya kupata keki hiyo ya Taifa ambayo Mheshimiwa Rais ameendelea kuigawa katika maeneo yote ya Tanzania. Tunamshukuru lakini tunampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amefanya kazi kubwa sana, amebadilisha fikra za Watanzania, ameendelea kuwafanya Watanzania kuwa na imani na Serikali yao, kuwa na imani na viongozi wao na kazi kubwa aliyoifanya ya kuwasikiliza wananchi kero zao. Kitu hiki alichokifanya atalipwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu mtu anapokuwa amejawa na mambo kifuani, tiba pekee ni kupata mtu ambaye atampa sikio na kumsikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Mheshimiwa Waziri Mkuu amelifanya kwa umakini mkubwa sana, ametoa tiba kwa Watanzania tena wa hali ya chini kabisa na Mwenyezi Mungu kama nilivyosema atamlipa kwa kadiri ya haya aliyoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki alichokifanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kimesababisha mabadiliko kwa watendaji kule chini, sasa katika baadhi ya maeneo wameanza kusikiliza kero za wananchi. Wameanza kuwasikiliza kwa sababu wameona Kiongozi Mkuu wa Kitaifa ameanza kufanya kazi hiyo, kwa hiyo na wao wameanza kuifanya kwa vitendo katika maeneo yao. Ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na kumshukuru sana kwa jambo hili ambalo analifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza sasa kwenye mchango wangu. Sisi Watanzania wote ikiwemo Wabunge tuliopo hapa ndani, wote tunatambua kwamba Mheshimiwa Rais amekuwa champion wa nishati. Siyo tu nishati ya kupikia, lakini nishati kwa ujumla wake na katika kuthibitisha hilo tumeona katika uongozi wake, awamu iliyopita amefanya kazi kubwa sana ya kuokoa maisha ya Watanzania ambao tunaambiwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, takribani wanawake 33,000 walikuwa wakipoteza maisha kwa mwaka kwa sababu ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuja na nishati safi ya kupikia na tumeona akina mama katika maeneo mbalimbali wameipokea, imewafikia. Kwa hiyo, hii unaona ni kwa namna gani Mheshimiwa Rais ameonesha moyo wa huruma, moyo wa upendo kwa wanawake wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi tulishuhudia hapa Tanzania, Januari 27 mpaka 28 hapa Dar es Salaam, tulikutanisha Wakuu wa Nchi za Afrika kwa ajili ya kujadili mustakabali wa nishati Afrika na moja kati ya maazimio yalikuwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkutano ule ulitambulika kama “Mission 300” na mkutano ule, kwa nini walikuja Tanzania? Ni baada ya kubaini kwamba, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme mpaka vijijini. Sasa walikuja Tanzania, kwa ajili ya kujifunza nini tunafanya mpaka kuweza kufikia hatua zile ambazo tumezifikia. Walijifunza na waliweka maazimio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mkoa wa Lindi tumekuwa sehemu ya wanufaika wa nishati na vijiji vyote 523 vya Mkoa wa Lindi tayari vimefikiwa na umeme. Sasa hii ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na umeme na kila mwanamke anapata nishati safi ya kupikia; unapozungumza umeme, unazungumza nishati safi ya kupikia. Pamoja na jitihada hizi za Mheshimiwa Rais, lakini kule Lindi umeme umekuwa kama koroboi, kwa wasiojua koroboi wengine wanaita kibatari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unakatika zaidi ya mara 10 au 20 kwa siku. Sasa je, ile dhamira ya kumkomboa mwanamke anayetumia nishati chafu ya kupikia tunaifikia, hatutaifikia? Je, ile dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na umeme hatuwezi kuifikia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kwamba, Serikali inaendelea kufanya jitihada, mikoa yote Tanzania imeungwa kwenye Gridi ya Taifa isipokuwa mikoa mitatu tu; bado Mikoa mitatu, ikiwemo Lindi na Mtwara. Naomba, pamoja na jitihada za Serikali, sisi Mkoa wa Lindi tuungwe kwenye Gridi ya Taifa, ndiyo uhakika pekee wa kuwa na umeme wa uhakika. Wanawake wa Mkoa wa Lindi wamenituma, wanaomba hii kero ya umeme wanayoipata, siyo tu inasababisha wawekezaji kutokuja katika mkoa wetu, lakini inaendelea kuharibu bidhaa za watu kwa sababu, umeme ukikatika, ukiwaka, ni kero kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba, Mheshimiwa Rais anayo dhamira ya dhati na nimesimama hapa kumwomba aendelee kutufikiria wananchi wa Lindi. Gridi imefika mpaka Mkoa wa Ruvuma na tunajua mkandarasi yuko kazini, lakini anakwenda taratibu sana. Umeme kuutoa Tunduru, Masasi mpaka Mahumbika ni kipande kidogo tu, tunaomba watufikirie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la migogoro ya wakulima na wafugaji. Wanawake wa Mkoa wa Lindi wamenituma, wanasema wanawapenda sana wafugaji, wanaipenda sana mifugo, lakini inaleta adha kubwa sana kwao kwa sababu, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima kwa asilimia kubwa, kwa hiyo, ninajua muda wangu unaelekea ukingoni, ninaomba. Pamoja na kwamba, tunawapenda wenzetu, tumeona kule Morogoro Mheshimiwa Rais mwaka jana, kama sikosei, alizindua mpango mzuri sana wa “Tutunzane”; tuufuatilie mpango ule kama umeleta manufaa twende tukautumie katika maeneo mengine ikiwemo Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili namwomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, baba yangu, kipenzi cha moyo wangu kabisa, Mheshimiwa Bashiru Ally, tuongozane kwa sababu, unapofika Mwezi Juni mpaka Mwezi Desemba hali kule Lindi inakuwa ngumu, akina mama wanateseka. Ukienda kwenye eneo linalopita Mto Mbwemkuru, Kilwa, Liwale, Nachingwea na Ruangwa, akinamama wanaishi kwenye taharuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi hawalali, kwa ajili ya kuhakikisha akina mama wanakuwa salama. Mkuu wetu wa Mkoa, Mama Telack, anahangaika kuhakikisha kwamba, akina mama wale wakulima wanakaa kwenye hali nzuri. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Bashiru twende akaone kuanzia Mwezi Juni mpaka Desemba jinsi akinamama wale wanavyoteseka. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Bashiru amesikia. Naomba maliza hoja yako. Unga mkono hoja. (Makofi)
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)