Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. JAMILA MAHMOUD JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya na uzima kuweza kuwepo hapa sasa hivi. Pia, nitoe shukrani zangu za dhati kwa chama changu, Chama Cha Mapinduzi kwa kunipa au kuniteua kuwa Mbunge ili kuja kujumuika na Watanzania wenzangu katika kuhakikisha kwamba tunaleta maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mkosefu wa shukrani pia, kama sitatoa shukrani zangu za dhati kwako pamoja na Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mjadala wa hotuba ya Mama, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; hotuba ambayo aliitoa wakati wa kufungua Bunge la Kumi na Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli hotuba ilijaa maono, lakini pia ilikuwa inaonesha dira na mwelekeo wa Taifa letu. Kama ilivyobainishwa kwenye ile hotuba yenyewe Mama mwenyewe aliweza kusema kwamba tunasonga mbele kujenga uchumi jumuishi unaogusa maisha ya kila Mtanzania. Kauli hii inaendana moja kwa moja na ilani ya uchaguzi inayolenga ustawi wa wananchi. Pia inaelezea dhima ya Taifa na maridhiano ya kitaifa ambayo hutoa huduma bora kwa jamii na uchumi wa uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba aliyoitoa Mheshimiwa haikuwa ya kawaida, ni hotuba ambayo ilijaribu kuunganisha siasa, uchumi, jamii na utu wa Mtanzania. Hivyo, mchango wangu utaangaza zaidi katika mambo tofauti ambayo Mheshimiwa Rais aliazimia wakati anatoa hotuba yake hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ninatokea kwenye Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI, mchango wangu nitaanza kuuelekezea kutokea huko. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais imeweka msisitizo mkubwa katika masuala ya ajira, lakini uboreshaji wa maslahi kwa wafanyakazi, madaktari, wauguzi na wahudumu katika vituo vya afya. Hili limedhihirishwa wazi kupitia ziara ambayo tuliifanya jana Kamati ya Kudumu ya Afya tulienda kutembelea Hospitali ya Dodoma na tuliona mazingira yalivyokuwa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji walisifia kwamba huduma ambazo wanazitoa zimetokana na sera pamoja na matakwa ya Mheshimiwa kwa sababu wamewezeshwa kwa vifaa vilivyo bora, maslahi yao yameongezeka, lakini pia na wao wameweza kutoa huduma kwa ufanisi kwa kuzingatia haki na bila upendeleo. Watu wote wanapata huduma na tuliona kwamba wameweza kuokoa maisha ya watu wengi pale hospitali tuliona kuna wodi ya watoto njiti, kuna watoto karibu 40 wako pale. Hii inaonesha kwamba kwa namna gani wameweza kuokoa maisha ya hawa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji pia, walitueleza kwamba wameweza au wanaweza kufanya upasuaji kwa watu 60 kwa siku moja. Hii inaonesha kwamba ni namna gani huduma za afya zimeimarika na zimeongezeka kiasi cha kwamba inatoa fursa kwa kituo kimoja kuweza kuwahudumia watu 60 kwa wakati mmoja, kwa ajili ya kupata operation na huduma nyingine ambazo zinatolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize kitu kimoja kwamba hatupaswi kupima mafanikio ya afya kwa majengo peke yake bali tunatakiwa tuangalie ubora wa huduma ambao tayari umeonekana kwa baadhi ya taasisi au hospitali ambazo tulizitembelea. Pia muda wa kusubiri wagonjwa, tumeona kwamba kwa sababu hospitali zimekuwa za kutosheleza kubwa na nyingi, kwa hiyo hata muda wa wagonjwa kusubiria umepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa dawa, tulijaribu kuongea na wagonjwa wawili, watatu ambao tuliwakuta pale wamesema kwamba wanashukuru kwamba dawa zinapatikana, lakini pia wagonjwa wamekuwa wakiheshimiwa. Yale malalamiko ambayo yaliyokuwepo huko nyuma, wakilalamika kwamba labda wagonjwa wanadharauliwa hawapati huduma vya kutosha, sasa hivi malalamiko hayo yameondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuishauri Serikali na watendaji ambao tunamsaidia mama katika utekelezaji wa ilani hii. Ili tuweze kuendelea katika kuwezesha si kwenye miundombinu tu, lakini tuna haja ya kufanya kazi na jitihada kubwa katika kutoa motisha, lakini kuhamasisha maadili na mazingira bora ya kazi kwa wahudumu wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nililoliangazia ni suala la ilani ya chama. Tumeona kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais iliendana sambamba na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Katika utendaji wa Serikali kupitia utekelezaji wa ilani hiyo tunaona kwamba uwezeshaji wa wanawake na vijana kupitia mikopo; kwamba Serikali imeahidi kuendelea kutoa mikopo kwa ajili ya akinamama na vijana. Kama alivyotangulia msemaji mmoja huko nyuma kwamba wanawake sasa hivi wamewezeshwa na wanaweza hii yote inatokana na maono ya mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji mkubwa katika masuala ya reli, bandari, barabara na nishati; tumeona kwamba kwa kipindi cha uongozi wake mama masuala ya usafirishaji kupitia reli, bandari lakini pia anga umeongezeka na watu wengi wamekuwa wakinufaika na miundombinu hiyo. Vilevile, viwanda vya kati na vidogo vimeongezeka. Pia suala zima la elimu ya ufundi na TEHAMA ambayo imezungumziwa kwa mapana yake ndani ya hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ninapenda kusema kwamba utekelezaji wa ilani lazima uambatane na masuala ya uwazi, ufuatiliaji na upimaji wa matokeo halisi kwa wananchi. Pia, nichukue fursa hii kuishauri Serikali na Bunge kwa pamoja kuwa mfano wa kufuatilia kila ahadi iliyomo kwenye ilani, kwa sababu kwa namna ya kutoa ripoti kwa wale watendaji tukiwa tuna utaratibu wa kutoa ripoti kila baada ya muda basi tuhakikishe kwamba tunafanya hivyo ili kuweza kuona ule mwendelezo na yale matokeo ya zile ahadi ambazo zilitolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake na vijana kama tunavyojua ni nguvu ya Taifa na tumeambiwa kwamba vijana wako 60% ya Watanzania wote, lakini wanawake ni 52% kama sikosei. Mheshimiwa Rais anaamini na anajivunia kwamba nguvu ya Taifa letu ni nguvu kutoka kwa vijana na wanawake. Hivyo, niombe kwamba tusimwangushe, tumuunge mkono katika hili kwa sababu kama wanawake tutasimama imara lakini na vijana pia kwa pamoja tukashirikiana kusaidia maendeleo ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa hotuba na ilani wanawake ni lazima washirikishwe katika kupanga na kusimamia program za Uchumi, lakini pia, Mifuko ya Uwezeshaji iwafikie wanawake na vijana hasa wanawake wa masokoni, mashambani na viwandani. Pia, vijana wa mijini na vijijini wapate fursa sawa katika hizi fursa za mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali haiwezi kufanya kazi peke yake, tumeona kwamba kuna hizi asasi za kiraia. Na-declare kwamba mimi ni Mbunge ambaye ninasimama kwa nafasi za NGOs na ushirikishwaji wa Serikali na NGOs kama utakuwa mzuri zaidi na tunaamini upo wa kutosha, lakini tunaomba, ushirikishwaji uwe wa karibu zaidi ili kuwafikia jamii za pembezoni. Kama tunavyojua kwamba hizi asasi za kiraia zinafanya kazi zaidi na watu au jamii ambayo ipo chini zaidi. Pia, hizi asasi za kiraia zitumike in a positive way katika kutoa elimu ya biashara, masuala ya afya ya jamii na masuala ya mazingira na pia kuwaunganisha wananchi kwa fursa za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ianzishe mifumo rasmi ya ushirikiano na NGOs katika utekelezaji wa masuala ya afya, uwezeshaji wa wanawake, ajira kwa vijana na ulinzi wa mazingira. Tukiwashirikisha wadau hawa utekelezaji utakuwa wa haraka, haki na gharama nafuu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni bila utekelezaji ni ndoto, hivyo, ninaomba tuwe na ripoti za utekelezaji za robo mwaka kwa kila Wizara; miradi ipimwe kwa muda, gharama na matokeo; ajira zipimwe kwa idadi ya vijana wanaoajiriwa na waliojiajiri wenyewe; na huduma zipoimwe kwa kuridhika kwa wananchi hapo ndipo Bunge litaona nafasi ya kweli litapokuwa na nafasi ya kweli ya kuisimamia Serikali kwa maslahi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. JAMILA MAHMOUD JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niunge mkono hoja, ahsante. (Makofi)