MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaungana na wenzangu kumtakia heri ya kuzaliwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaishukuru Serikali kwa kutuletea mkandarasi wa kujenga Barabara ya lami kutoka Kyerwa kwenda Omurushaka, kilometa 50. Hata hivyo, speed yake ni ndogo sana. Je, Serikali ina mkakati na maelekezo gani ya kumsimamia mkandarasi huyu ili amalize barabara hii ili kukidhi kilio cha wananchi wa Kyerwa? Ninakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli mkandarasi huyu anakichofanya ni sanifu jenga Barabara ya Kyerwa kwenda Omurushaka. Nimwagize Meneja na Mhandisi Mshauri anayemsimamia ahakikishe kwamba huyu mkandarasi, kwa sababu alikwishalipwa fedha ya awali, aweze kwenda kwa kasi inayotakiwa kulingana na mpango wake wa kazi ambao ameupanga na tumeukubali. (Makofi)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali hili la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia wahudumu 58 katika dirisha hili la ajira za afya kwa Wilaya ya Kyerwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Nkwenda ni kikubwa na kinatoa huduma zaidi ya Kata 19 na sometime kinatoa huduma nje ya Wilaya ya Kyerwa, lakini kituo hiki hakina gari ya uhakika ya wagonjwa (ambulance), je, ni lini Serikali itatupatia gari la uhakika kwa ajili ya kutoa huduma safi kwa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT.JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunakumbuka sote humu ndani katika kipindi cha miaka mitano Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 316, pamoja na magari ya wakaguzi 212 na ambulance za awamu ya kwanza tumeshazigawa katika Halmashauri ambazo ziliainishwa. Nimhakikishie kuwa, awamu ya pili kituo hiki kitakuwa wanufaika wa gari la ambulance.