Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khalid Mussa Nsekela (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na afya ya kuweza kuwa hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kukushukuru wewe hapo na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, hasa ya kuzunguka ndani ya Nchi ya Tanzania, mikoa mbalimbali na kutatua kero. Nichukue nafasi hii, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kyerwa, Mkoa wa Kagera kumwomba kwamba, angalau tunashukuru kama tutawekwa kwenye ratiba atutembele Mkoa wa Kagera na Jimbo la Kyerwa na sisi tuna kero nyingi sana, tunapenda tumwambie uso kwa uso. Hili ninamshukuru Mheshimiwa Rais, ninakumbuka wakati anafungua Bunge hili alielekeza kwamba, uongozi wake utajikita sana kwenda kuwasikiliza Watanzania na kutatua kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kidogo kwenye hotuba hii nzuri kabisa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ninachangia maeneo matatu, eneo la kwanza ninaomba nichangie kwenye suala la barabara, miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatokea Jimbo la Kyerwa, sisi ni wakulima wa zao la kahawa, zao kubwa kabisa, zao la kimkakati. Sisi tuna athari kubwa sana kutokuwa na barabara nzuri, hasa barabara ya lami, barabara za vijijini. Kutokuwa na barabara za vijijini ni tatizo kwa sababu, tunatambua kwamba, barabara siyo tu kwa ajili ya kusafirisha mazao na watu, lakini ni uti wa mgongo wa huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia suala la afya, Mheshimiwa Rais ameleta vituo vya afya vya kutosha. Tunavyo vituo vya afya vitano katika Jimbo la Kyerwa, lakini kitendo cha kutokuwa na barabara imara inakuwa ni changamoto kwa mwananchi kutoka nyumbani kwake kwenda kupata huduma kituo cha afya kwa sababu, hawezi kupita ile barabara na hasa katika hali hii ya mvua, unakuta kuna sehemu huwezi kuvuka. Mvua ikianza lazima wananchi wakae hapo mpaka iishe ndiyo waweze kuvuka. Barabara kama sehemu za Munchwekano kule, ukienda Kihea, ukienda Rwabwere, vijiji ni vingi sana ukisema uvitaje huwezi kupata muda wa kutosha, lakini barabara zile ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vilevile kwenye suala la kilimo. tunajua wakulima, ili waweze kupata tija ni lazima waweze kupeleka mazao yao sokoni. Kitendo cha kutokuwa na barabara imara, mkulima anapata changamoto na sana sana, tunakuja kupata tatizo la post harvest loss, mazao mengi sana hayafiki sehemu za masoko. Barabara ni muhimu sana na katika suala la uchumi wa Tanzania nzima, tumeona nchi nyingi sana zimetoka hatua moja kwenda hatua nyingine baada ya kuwa na miundombinu imara ya barabara, tunatambua hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maji. Tunatumia gharama nyingi sana kupeleka mitambo, sijui wataalam kwenda kutengeneza miradi ya maji, lakini kitendo cha kutokuwa na barabara ni shida kubwa sana, hasa katika Jimbo la Kyerwa ambalo jiografia yake kidogo imekaa vibaya, milima na mabonde. Kutokuwa na barabara unakuta ni changamoto sana kupeleka miradi sehemu ambayo inatakiwa kwa sababu, wataalam wa mradi huo hawawezi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kuhudumia ile miradi vilevile inakuwa ni ngumu pale tunapokuwa na changamoto ya hiyo miradi. Kwa hiyo, rai yangu ni kwamba, tunaomba TARURA iongezewe nguvu ya kuweza kuhudumia hizi barabara, tunatambua umuhimu wake, tunatambua umuhimu katika uchumi na katika kutoa huduma. Tukiwa na barabara imara hatutatumia gharama nyingi kupeleka zile huduma pale zinapotakiwa. Ninatoa rai kwamba, ni muda sasa hizi halmashauri ziongezewe nguvu na kujengewa uwezo wa kuhudumia hizi barabara za TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni sehemu ya vijana. Tunatambua tuna zaidi ya 60% ya vijana katika nchi hii. Hii ni asset kubwa sana kwa Nchi ya Tanzania, hasa tunapojiandaa kwenda katika Dira yetu ya 2050. Tukiwekeza vizuri katika hawa vijana, tukawapa ujuzi na tukawatengeneza, tunaamini kabisa kwamba, sisi tutafika vizuri katika hiyo dira yetu na hapa namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada na initiative ambazo amezifanya katika kumkomboa na kumnyanyua kijana wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ameanzisha Wizara ipo chini yake, lakini bado ametoa shilingi bilioni 200 ambazo nyingi zinaenda kwenye sekta ya vijana. Hii ni dhahiri kwamba, Mheshimiwa Rais ana maslahi mapana ya vijana wa Tanzania. Mimi hapa, kama kijana, ninaomba nitoe rai kwamba, hizi hela zinakwenda kwa vijana ambao tayari wameanza kuwa na biashara ndogondogo kuwawezesha kuwa na mtaji mdogo, lakini wapo vijana wengi sana mtaani ambao hawana uwezo wa kuanza biashara hata ndogondogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu ni kwamba ni muda sasa hizi halmashauri ambazo ziko mikoani na halmashauri zote nchi nzima ziwe na kitengo ambacho kitawaruhusu vijana waje pale watoe mawazo yao yanayohusu TEHAMA, kilimo na biashara. Halafu sasa Serikali ione ni jinsi gani ya kuwezesha yale mawazo ili kuwanyanyua, kwa sababu tunajua wapo vijana wengi, tukiwawekea chumba maalum bila hata kuwalipa na kuwaambia vijana njooni hapa, toeni mawazo yenu ya TEHAMA, kilimo, biashara, chochote wewe elezea, wazo lako likoje wataeleza. Tukae pamoja, tuwape na mwalimu au mentorship wa kuwaongoza vizuri, tutapata mawazo mazuri, tutaweza kuanzisha vijana ambao tayari watakuwa kwenye biashara na kuendelea juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, ninaomba nichangie kwenye suala la dira kulingana na hii hoja au hotuba ya Waziri Mkuu. Hii ni bajeti ya kwanza kuelekea Dira ya 2050 na ninamshukuru sana Waziri Mkuu ameelezea vizuri uelekeo wa Dira hii ya 2050, lakini hoja yangu ni jinsi gani mipango yetu inaakisi hii Dira ya 2050? Je, sekta zetu zote zinajielekezaje kumfikisha Mtanzania wa leo kwenye 2050? Kwa sababu tunapokaa hapa Bungeni ninaona kabisa Mawaziri wetu, ukimwona Waziri Profesa Shemdoe na timu yake wapo kwenye field wanahakikisha tupate matokeo lakini nani yuko ofisini kwa ajili ya kuandaa TAMISEMI ya 2050?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwona Mheshimiwa Waziri Aweso anashughulika na maji ameenda China, amekuja wapi, lakini nani kabaki ofisini kuhakikisha kwamba Wizara ya Maji ya 2050 itakuwa hivi? Kwa hiyo, rai yangu hapa ni kwamba kuna haja sasa rasmi tuwe na kitengo maalum kwenye kila Wizara, kila Taasisi cha ubunifu na mabadiliko makubwa ya kuziandaa sekta zote za Tanzania kwa ajili ya 2050, maana yake ninasema future ready economy au future ready government.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na vitengo ambavyo vinakaa ofisini kwamba wakati hawa wako field wanafanya kazi hii, lakini hatoki kwenye mstari, tunataka sekta ya afya iwe hivi kwa 2050, sekta ya ujenzi, sekta ya maji, tuwe nazo tayari na mwelekeo mzuri ambao unatuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ninaomba tunapokuwa tunafanya kazi au Wizara zetu tunaambiwa Waziri Mkuu aje na ajenda ya kuchangamana au ku-incorporate hizi Wizara zishirikiane kwa sababu, kwa sasa unavyoweza kuangalia kila Wizara inafanya kazi pekee yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliwahi kuongea Mheshimiwa Musukuma pale, alitoa mfano mdogo akasema Barabara ya kutoka Airport kuja Posta - Dar es Salaam ina kona nyingi sana ambazo hazina umuhimu wa kuwa nazo. Lakini ukiangalia ni kwamba Wizara ya Ujenzi haina mahusiano na Wizara ya Utalii. Sisi tunavyotoka kwenda Dubai tunashangaa Barabara za Sheikh Zaid Road ni barabara tu. Kwa hiyo, barabara hii nayo ni utalii siyo mpaka uende msituni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara ya Kilimo au tubaki hapa kwenye Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ujenzi lazima ishirikiane na Wizara ya Nishati, siyo unajenga halafu ndiyo anakuja kuvunja anapitisha nguzo. Wizara ya Maji barabara imejengwa huyu anakuja kuvunja apitishe bomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa mfano tu Wizara ya Kilimo, lazima ikae na Wizara ya Elimu, haiwezekani muda huu hatuna graduate anaweza akasema au wanatoka graduate saa hizi wanakuja, hana elimu inayohusu madini. Wapo graduate hawana elimu kuhusu kilimo, wapo hawana elimu kuhusu utalii. Hii maana yake hatushirikiani Wizara ya Kilimo na Wizara ya Elimu kuona kwamba tunatoa graduates gani kwa ajili ya kuiandaa Tanzania. Uchumi wetu wote uko kwenye kilimo, upo kwenye utalii, upo kwenye madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni hayo ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)