Supplementary Questions from Hon. Josephine Joseph Kapoma (3 total)
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Je, Wizara ina mkakati gani wa kuja na solution ya kudumu, na hata kama siyo ya kudumu japokuwa ya muda mrefu kwa zile barabara zinazozibwa viraka? Kwa mfano, kuna baadhi ya barabara unakuta zina mashimo, lakini zinazibwa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninataka kujua kama tunaweza tukapata solution ya kuziba viraka ambavyo vitakaa kwa muda mrefu kwa ajili ya ku-save pesa ambazo zinatumika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge wa Mkoa mzima wa Morogoro aliyetoka kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo sisi TARURA ndani ya Serikali kwa ajili ya kuanza mkakati wa kutumia teknolojia mpya ambayo itajenga barabara zetu kwa gharama nafuu na hivyo tutaweza kuyafikia maeneo mengi na kujenga barabara zinazodumu kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa huu Mkoa wa Morogoro ambao Wabunge wake wameuliza maswali mengi hapa, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, tumejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami na sasa tumefikisha karibia kilometa 125. Mradi wa TACTIC ambao tulitekeleza kwa awamu ya kwanza tulipeleka zaidi ya shilingi bilioni 19. Mheshimiwa Rais lengo lake ni kutaka kuona anaufungua Mkoa huu mkubwa ambao ni muhimu kwa uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nina swali dogo la nyongeza. Kama ikimpendeza Mheshimiwa Naibu Waziri atalijibu au atalichukuwa. Wilaya yetu ya Malinyi tumekuwa tuna shida ya gereza la mahabusu kwa muda mrefu sana. Eneo limepatikana lakini kumekuwa kuna ucheleweshwaji wa kukamilisha ambayo inawafanya wahusika kusafiri umbali mrefu sana kwenda Wilaya ya Ulanga. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamu ili niweze kujibu vizuri; amekusudia mahabusu ya polisi au ya gereza?NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu ya gereza.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaongelea kuhusu suala la Jeshi la Polisi lakini kwa sababu Magereza na yenyewe ni sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini ninaomba tu nimjibu Mheshimiwa Kapoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo baadhi ya magereza yamekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo. Hata hivyo, moja ya eneo ambalo amelitaja la jimbo lake kwamba wilaya nzima ya Malinyi hakuna gereza na kupeleka eneo la pili; tunakuja na mpango na tutaueleza kwenye bajeti ya mwaka huu kwamba ni mpango gani kwa upande wa Jeshi la Magereza, tutaenda kuboresha magereza katika maeneo ambayo yana uhaba likiwepo eneo lake la Malinyi.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wa Kata ya Boma Mlimani Luhungo wa Wilaya ya Morogoro Mjini wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu na Serikali kwa ajili ya uharibifu wa mazingira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na mkakati wa kutoa elimu ya mbinu bora za kilimo zitakazozingatia uhifadhi wa mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Josephine kwamba, moja ya mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba wananchi hawaendelei kuharibu mazingira, ni pamoja na kuhakikisha tunajenga miundombinu bora na ya kisasa, kwa maana ya mabwawa na schemes ili wananchi wale tukishawapanga na kuonesha maeneo ambayo wanafaa kufanya kilimo chao, maana yake hawatakuwa na nafasi ya kwenda kuharibu mazingira katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tutaendelea kupeleka timu kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira, kwa sababu sisi mazingira ndiyo ambayo yanatusaidia kupata vyanzo bora vya maji ambavyo sasa miradi yetu ndiyo maeneo ambayo tumekuwa tukitekeleza.