Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hasnain Gulamabbas Dewji (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HASNAIN G. DEWJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kupata nafasi. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Vilevile, ninawashukuru wananchi wangu wa Kilwa Kusini kwa kuniamini na kwa kunirudisha tena kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujumbe ninaowapa wananchi wangu wa Kilwa ni kwamba, sitawaangusha. Kwa umri niliokuwanao, lazima nitaweka alama pale Kilwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu mpendwa, kwa kuniamini kunipa nafasi hii ili niweze kumalizia nafasi yangu ya Ubunge. Ninamshukuru sana Mama kwa kuleta maendeleo makubwa Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yake Waziri Mkuu ameitaja Bandari ya Kilwa Masoko, Bandari ya Samaki. Hii bandari ni ya mfano. Kwa Bahari ya Hindi, hakuna bandari kubwa ya uvuvi kama Bandari ya Kilwa Masoko. Serikali imetumia shilingi bilioni 280, fedha ya ndani. Hii fedha yetu ya ndani siyo ya mkopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya bandari hii kujengwa samaki wetu walikuwa wanatoroshwa kupelekwa nchi za Ulaya. Samaki wengi wamekwenda Europe kwa kukosa bandari; facility, hazikuwepo. Ukiwakamata wanakwambia, hakuna huduma kwenu, wanawatorosha samaki. Serikali sikivu imeona hili, tumepata bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari hii ya kipekee bado iko kwenye 90%. Mungu akijalia, mwezi wa Sita Mama atakuja kuizindua, wateja wengi wanaiulizia hii bandari. Kuna wawekezaji wa Somalia wako tayari kuitumia Bandari ya Kilwa Masoko, wataleta mzigo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakwambia Kilwa kuna samaki jodari, kwa kiingereza wanaitwa tuna fish wenye nyama nyeupe, wanapatikana katika Bahari ya Hindi peke yake. Kwa hiyo, hawa samaki ni adimu sana, lakini samaki wote walikuwa wanatoroshwa kwenda Europe. Kwa hiyo, tunaishukuru Serikali kuliona hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari hii itatumika, watu wa Msumbiji wataitumia, Tanzania tutaitumia, Kenya wataitumia, Somalia wataitumia. Mpaka sasa hivi Wasomali wameshakuja kuniona, wapo tayari kuleta meli nne kila mwezi walete samaki, baadaye wasafirishwe kwenda nchi jirani kama Zambia, Congo na South Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaishukuru sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan. Hii ni hazina kubwa kwetu Kilwa, italeta ajira kubwa, tunategemea watu 3,000 watapata ajira pale. Ni fursa kubwa, ninawahakikisha watu wa Kilwa wataanza kupata fursa hiyo ya ajira kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tuna upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko. Kwa kuwa ipo bandari, inabidi tuwe na airport kubwa. Kwa hiyo, airport inajengwa, lakini tuna tatizo la fidia. Kuna wananchi pale hawajalipwa fidia. Suala hili Waziri Mkuu analijua, alikuja kututembelea. Kwa kuwa, Serikali yetu ni Sikivu ninawaambia wananchi wangu wanisikilize, mboga ipo jikoni, mtalipwa. Shilingi bilioni 6.2 zinadaiwa kwa ajili ya fidia ya uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, Songo Songo tunatoa gesi ya kutosha, na TPDC mwaka huu wanaongeza visima viwili, lakini tatizo kubwa ni la mrahaba. Mwaka 2008 nilikuwa Mbunge wa kwanza kutetea mrahaba, Serikali wakati huo tukaanza kupata mrahaba kutokana na gesi asilia ya Songo Songo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2025 wakati ninakwenda kuomba kura Kijiji cha Songo Songo wananiambia hawapati kitu. Ninataka nijue, huo mrahaba nilioutetea miaka hiyo, bado upo? Kwa nini mrahaba hauendi Halmashauri? Kwa nini mrahaba hauendi kijiji husika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mradi wa mbolea, TPDC walitupa kiwanja Kilwa Masoko ili gesi asilia itumike kwa ajili ya kiwanda hicho cha mbolea. Ninataka nijue huo mpango wa kuleta hicho kiwanda umefikia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaelekea upande wa maji. Tunaishukuru Serikali, tumepata Mradi mkubwa wa Maji wa Mavuji, unasaidia Kijiji cha Nangurukuru, Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko. Ninatumaini ule mradi umefikia 80%. Nilikuwa ninaiomba Serikali, tupate extension vijiji vya jirani. Kuna Kijiji cha Kiwawa, Hoteli Tatu, Mandawa na Mtandi, havina maji. Kwa hiyo, ninamwomba Waziri katika mradi huo tupate extension, hivyo vijiji navyo vinufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongelea kuhusu tembo. Wilaya ya Kilwa ipo jirani sana na Selous, tunapata tatizo kubwa sana. Halmashauri imenunua drone moja tu wilaya nzima. Tuna majimbo mawili, tuna drone moja, haiwezi kusaidia. Kwa kuwa, halmashauri inashindwa uwezo, ninaiomba Serikali Kuu, tuwe na drone za kutosha. Wananchi wetu, na wakulima wetu, wanapata hasara kubwa sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Malizia, muda wako umeisha.

MHE. HASNAIN G. DEWJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)