Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yumna Mmanga Omar (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. YUMNA MMANGA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima, lakini kwa kunipatia kibali cha kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge hili la Kumi na Tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa heshima kubwa nipende kumshukuru kipenzi chetu Mama yetu, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha nimshukuru pia Mama yetu, mlezi wetu Mama Mary Pius Chatanda, kiongozi na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania kwa uongozi wake ulio thabiti na kutulea sisi mabinti na wanawake ndani ya jumuiya hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo sasa nielekee moja kwa moja kwenye kuchangia hoja iliyopo mezani ambayo ni hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi nitagusia vipengele viwili ambavyo ni sekta ya elimu na sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakwenda moja kwa moja nipende tu kuipongeza Serikali kwa hatua kubwa za maendeleo inayoendelea kuzipiga katika sekta hizi. Pia, kama Taifa tulipo sipo tulipotoka, lazima tukiri hilo ila sipo tunapotaka kufika. Kwa hiyo inatulazimu tuseme ili tuweze kufikia kule tunapotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, inazungumzia kwamba kupitia Wizara ya Elimu, Serikali imetenga shilingi bilioni tisa kwa ajili ya ufadhili wa wanafunzi kwa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, sambamba na Hisabati ambapo Serikali imefadhili wanafunzi 1,786. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetoa pia shilingi bilioni tano kwa Samia Super Scholarship Fund kwa wanafunzi 50 bora kwa sekta ya akili unde na Sayansi data. Hapa napatwa na maswali, kwenye ufadhili huu wanafunzi wenye ulemavu wamefikiwa kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba, ndugu zetu watoto wetu wenye ulemavu wanakumbana na changamoto mara tatu zaidi kuliko wanafunzi wengine, kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu na ndiyo maana hata ukitazama takwimu zimejichora kabisa pyramid kwamba huku ngazi ya chini wanakuwa wengi, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu, vifaa saidizi, uelewa, mazingira, vinawarudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kumwangalia mwanafunzi mwenye ulemavu ambaye amepata division two, ukam-recognize sawasawa na asiyekuwa na ulemavu ambaye ana division one. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila shaka huyu ametumia nguvu mara tatu zaidi afikie pale highest of his/her potential. Kwa hiyo, ni ombi langu kwa Serikali kuhakikisha kwamba fursa hizi tunaweka mikakati madhubuti (affirmative measures) ambazo zitaongeza ushiriki wa wanafunzi wenye ulemavu kwenye fursa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia science technology engineering and mathematics ni uchumi wa nchi, tunapoliacha kundi hili nyuma, maana yake tunawaacha nyuma katika ushiriki wao wa uchumi ndani ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea mbele nigusie sekta ya afya; ambapo tumeona Serikali kwa kuimarisha ubora wa sekta ya afya nchini, imesomesha madaktari bingwa na bingwa bobezi kwenye kada mbalimbali. Nipende tu kutoa ushauri wangu kwa Serikali kwamba madaktari hawa waende wakagusie kada ambazo zinatugusa sisi watu wenye ulemavu moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaathiriwa na mionzi ya jua; mionzi hiyo hupenya hadi kupitia kioo, hata kunapokuwa na mawingu ya mvua, bado hupita. Hivyo basi, ninahitaji kuwa na periodic check up ambazo zitaniwezesha kuangalia uwezo wa ngozi yangu, kwa kuwa ninafanya kazi siwezi kuepuka jua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama binadamu ninakonda, ninanenepa, ninakua ule mguu bandia ambao umenipatia unaweza ukawa haunitoshi ni lazima niende kwa daktari kila baada ya muda akaangalie, aniongezee, anipunguzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wenye ulemavu wa uziwi pia wanahitaji kwenda kwa daktari kuangalia zile shime sikio waliozopatiwa zinawasaidia? Wapewe nyingine. Ndiyo maana idadi kubwa ya ndugu zetu wenye ulemavu wa uziwi hawataki kutumia shime sikio kwa sababu madaktari hawa hawapo ni pungufu kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ni mapendekezo yangu kwa Serikali kuhakikisha kwamba wanaongeza madaktari bingwa kwenye kada hizi ili kupunguza, lasivyo tutakuwa tunaongeza intensity ya ulemavu kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kwamba, tunapoandaa bajeti zetu tuhakikishe kwamba hizi bajeti zinakuwa inclusive budget ili katika kila eneo tuone ni kwa namna gani tunatenga fedha kuwajumuisha watu wenye ulemavu kwenye sekta ya afya, kwenye sekta ya elimu, kwenye sekta ya michezo katika kila eneo pamoja na zile key performance indicators ili tuone kama Taifa tuko wapi na tunahitaji kwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, sisi kama Taifa, sisi kama Wabunge humu ndani kila mmoja ana haki na wajibu wa kuzungumzia watu wake, nami kwa niaba ya watu wenye ulemavu, ninaunga mkono hoja pamoja na mapendekezo hayo. Ahsante. (Makofi)