Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Twaha Said Mwakioja (2 total)

MHE. TWAHA S. MWAIKOJA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Taasisi zetu za Serikali za TANAPA, NCAA na TAWA zinabaki na mapato ili kuweza kutoa huduma mbalimbali. Pamoja na kubaki na mapato (retention) bado tumekuwa na changamoto ya kuwapa waathirika hawa wanaokumbana na majanga haya ya wanyamapori kifuta jasho ambacho ni kidogo na kiwango hiki ni cha muda mrefu sana. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya mapitio juu ya viwango hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; utaratibu wa kufanya uthamini kwa wananchi wanaopata majanga umekuwa na urasimu mkubwa sana na kusababisha baadhi ya wananchi kushindwa kufuatilia na kuendelea kuilalamikia Serikali yetu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya mapitio juu ya mchakato huu ili uwe rahisi na kuwaletea tabasamu wananchi wetu na hususan wananchi wa Jimbo la Mkinga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Twaha Mbunge wa Mkinga, ninaomba nimpongeze sana pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuaminiwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ilishafanya marekebisho ya Kanuni ya Mwaka 2011, kanuni hiyo ilionekana ni kweli kifuta jasho ni kidogo imefanyiwa marekebisho mwaka 2024 kwa Tangazo la Serikali Na. 440, mwaka 2024, tarehe 31 Mei na imefanya marekebisho makubwa. Kwa sasa waathirika wale ambao watakuwa na ulemavu wa muda mfupi yaani majeraha ya muda mfupi watalipwa 50%, vifo vya mifugo 50%, uharibifu wa mazao 50%. Pia lipo ongezeko kubwa la vifo na ulemavu wa kudumu kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali tayari imeliona hilo suala la urasimu na kwa sasa tunatumia mfumo maalum unaotambulika kwa jina la PAIS yaani Problem Animal Management Information System ambao sasa urasimu hautopatikana, maana yake inarekodi moja kwa moja na kuhakiki taarifa zile na kupelekwa kwenye kanzidata. Nina imani kabisa kwamba urasimu huo sasa utakuwa umepata mwarobaini wake. Ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri. Pamoja na majibu hayo mazuri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mradi huu wa kihistoria ambao kwa Wilaya ya Mkinga haujawahi kutokea. Pamoja na hivyo mradi huu unatekelezwa kwa kusuasua sana. Wananchi wa Mkinga wameyasubiri maji haya kwa muda mrefu, tarehe za ukamilishwaji wa mradi huu zimekuwa zikibadilishwa kila mara. Pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuwa mradi huu tangu mwaka jana ukamilike pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kwamba mradi ukamilike, lakini mradi huu haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia ni kwamba mkandarasi anaidai Serikali na alishasimama akaondoka eneo la mradi; je, Serikali ina kauli gani kuhusu kumlipa mkandarasi huyu ili tarehe iliyotajwa ya kukamilisha mradi huu mwezi Julai iweze kutimia na wananchi wenzangu wa Mkinga waweze kupata maji safi na salama waliyoahidiwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Mkinga inatarafa mbili, mradi huu wa kihistoria na mzuri unakwenda kuwapatia maji watu wa Tarafa moja ya Mkinga. Hali ya Tarafa ya pili ya Maramba katika upatikanaji wa maji ni mbaya mbaya kweli kweli. Wakati wa kiangazi walifikia hadi kununua dumu la maji kwa shilingi 3,000 mpaka shilingi 5,000.

Je, kaka yangu Waziri wa Maji yupo tayari kuambatana na mimi katika kipindi hiki cha bajeti ili tukaione hali ya Tarafa ya Maramba na ikiwezekana atafute vyanzo vipya vya maji na ikibidi basi atuunganishe na Gridi ya Maji ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Mkinga kwa kazi nzuri kwanza kabisa ya ufuatiliaji wa miradi. Kwa namna alivyoongea inaonekana anafuatilia hatua kwa hatua na kujiridhisha changamoto iko wapi. Sisi Serikali kupitia Wizara ya Maji tumejipanga kuhakikisha miradi mingi ya maji inakamilika ukiwemo mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameongelea mradi huu ni wa kihistoria. Ni kweli kabisa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza shilingi bilioni 35.4 kuhakikisha kwamba eneo la Mkinga linapata suluhisho la kudumu. Vilevile, Serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi bilioni 1.5 lakini pia ndani ya mwezi huu mkandarasi tunaenda kumlipa shilingi bilioni 1.7 arejee na kuendelea na mradi ili uweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kiu ya Mheshimiwa Mbunge na Wana-Mkinga ni kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanatatuliwa kuhakikisha kwamba wanapata huduma ya maji safi na salama, lakini tuangalie upatikanaji wa maji mpaka sasa kwa Wilaya ya Mkinga ni 72.9% na kuna vijiji 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji 85, vijiji 52 vyote vina maji isipokuwa vijiji 23. Katika vijiji 23 Serikali tumejipanga kuendelea kutafuta fedha ili vijiji 23 vya Mheshimiwa Mbunge ikiwemo Maramba ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tutaingiza kwenye mpango wa bajeti ili twende kuhakikisha kwamba Wana-Maramba kwa sauti ya Mbunge wao wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)