MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza:-
Je, ni lini Tembo wanaojeruhi na kuharibu mali majumbani na mashambani maeneo ya Mwakijembe, Bwiti, Daluni na Duga watadhibitiwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninaomba kumshukuru sana sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kuingia katika awamu hii tukiwa salama.
Mheshimiwa Spika, pili, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini. Ninatoa ahadi kwamba nitafanya kazi kwa weledi mkubwa, uadilifu pamoja na ufanisi mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga. Mkakati huu unajumuisha kuweka vikosi vya kudumu vya askari katika Kata za Bwita na Mwakijembe kwa ajili ya mwitikio wa haraka wa matukio ya wanyamapori katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea pia kutumia teknolojia za kisasa hasa visukuma mawimbi (GPS Collars, ndege nyuki pamoja na mabomu baridi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika Wilaya ya Mkinga. Ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: -
Je, lini Serikali itawapatia maji safi na salama wananchi wa Wilaya ya Mkinga kupitia Mradi wa Tanga – Horohoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mkinga – Horohoro kwa gharama ya shilingi bilioni 35.4. Kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matanki 10 yenye jumla ya ujazo wa lita 2,450,000, ulazaji wa mabomba yenye umbali wa kilometa 223.7 sanjari na ujenzi wa vituo 58 vya kuchotea maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi wa Mkinga – Horohoro umefikia wastani wa 65% na umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kijiji cha Mtimbwani. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2026 na kunufaisha wananchi wapatao 57,334 waishio katika vijiji 37 katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.