Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yohana Stephen Msita (3 total)

MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itapeleka wataalam kwenye Jimbo la Itigi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu wa dengu ili waweze kuongeza tija zaidi kwenye zao la dengu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwa ajili ya kwenda kuongea na wale wakulima kwa sababu wana mambo mengi sana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nimpongeze Mheshimiwa Yohana Msita, Mbunge wa Itigi, ameanza vizuri kazi yake ya Ubunge, ni Mbunge mpya lakini unauona umakini wake. Nimthibitishie tu kwamba, moja, Serikali tutaendelea kupeleka wataalamu, lakini wale waliopo sasa hivi maafisa ugani, tutaongeza msukumo ili kuhakikisha wanafanya hiyo kazi kama ambavyo imekusudiwa kwa sababu lengo letu ni kuongeza tija ya zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mimi niko tayari kuongozana naye katika Jimbo la Itigi, uzuri hapa siyo mbali tunaweza tukaenda na kurudi. Kwa hiyo, niko tayari muda wowote ambao yeye Mheshimiwa Mbunge atakuwa na hiyo ratiba.
MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Itigi ninapenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri.

Kwa kuwa Jimbo la Itigi lina kata 13 na tunavyo vituo vinne tu vya afya na hili jimbo lipo scattered sana. Je, nini mpango wa Serikali kujenga vituo vya afya angalau kwenye kata tatu za Ipande, Mgandu pamoja na Mwamagembe ili kupunguza adha ya wananchi wangu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yohana, Mbunge wa Jimbo la Itigi kama ambavyo ameliuliza. Jimbo la Itigi ni miongoni mwa majimbo ambayo tumekwishayaombea fedha Hazina ili tuweze kujenga vile vituo vya afya vya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge nitampa ushirikiano wa dhati ili kuweza kuhakikisha angalu kwenye kata hizi tatu alizoziainisha ziweze kupata kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali langu. Naomba kuuliza kwamba, kwa kuwa athari ni kubwa katika Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kihanju, Sanjaranda, Gurungu, Njirii, Aghondi, Kamenyanga, Kashangu na Idodyandole; na kulingana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba wamevuna tembo wawili: -

(a) Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuendelea kuvuna angalau hata tembo 20 ili kupunguza adha kwa wananchi kwa sababu athari ni kubwa sana?

(b) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana pamoja na mimi ili kwenda kujionea hali halisi ya athari iliyopo Jimbo la Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Yohana, kwani sasa amekuwa ni sehemu ya hifadhi, na pia anakuwepo ofisini mara kwa mara kutetea wananchi wake kwa usumbufu ambao wanaupata kutokana na wanyamapori hawa wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli alichosema, kwamba Serikali imewahi kuvuna tembo wawili; na nimeona na nimesikia pendekezo lake kwamba tuendelee kuvuna, lakini kuvuna wanyama hawa ni lazima tufuate sheria, kanuni na taratibu. Kwa hiyo, tutaangalia taratibu, zikiruhusu, basi wale wanyama ambao wamekuwa ni wakali sana na ni waharibifu, inawezekana.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, mimi niko tayari kabisa kufuatana na ndugu yangu ili twende jimboni, tuone kadhia hiyo ili tuhami wananchi wetu, waweze kuendelea kuishi kwa tabasamu.