MHE. YOHANA S. MSITA aliuliza:-
Je, nini mpango wa Serikali wa kupandisha bei ya zao la dengu baada ya bei kuporomoka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mkakati wa kusambaza mbegu bora za dengu nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara imepanga kusambaza kilo 400 za mbegu mama za dengu kwa wakulima wa Halmashauri ya Itigi zenye uwezo wa kuzalisha tani nne za mbegu bora. Lengo ni kuhakikisha wakulima wanaongeza tija na uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa na kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali vilevile inaendelea na taratibu za kufungua soko la dengu Nchini Malaysia. Upatikanaji wa soko hilo utaruhusu zao la dengu kuingia rasmi katika soko la Malaysia. Hatua hiyo itaongeza wigo wa masoko na hivyo kuimarisha bei kwa mkulima.
MHE. YOHANA S. MSITA aliuliza: -
Je, upi mpango wa Serikali wa kuondoa kero ya wanyama waharibifu kama tembo kwenye Jimbo la Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Yohana Msita, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu katika Jimbo la Itigi, ikiwemo kuendelea kutumia kituo cha kudumu cha Askari kilichopo katika Kijiji cha Doroto na kambi za muda mfupi tatu kwenye Vijiji vya Chisingisa, Sanjaranda, na Kitaraka kwa ajili ya kuitikia kwa haraka kwenye matukio na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, kuendelea na kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu; kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mbinu rafiki za kudhibiti wanyamapori hao; kuendelea kugawa nyenzo na vifaa rafiki kwa wananchi ili kudhibiti na kuzuia wanyama waharibifu hao, tembo, kwa vijiji mbalimbali; kuendelea kutumia teknolojia ya ndege nyuki; na kuendelea kushirikiana na wadau.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Southern Tanzania Elephant Program (STEP) imetengeneza vihenge 24 vya kuhifadhi mazao yaliyoboreshwa. Sambamba na hatua hizo, Serikali imevuna tembo wawili waliokuwa wakihatarisha usalama wa maisha na mali za wananchi katika Vijiji vya Doroto na Sanjaranda.