Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ester Edwin Malleko (3 total)

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa TASAF imelenga kuwasaidia kaya maskini katika kupunguza umaskini katika hizo kaya, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inawapatia wale watoto waliotoka kwenye kaya maskini mkopo wa elimu ya juu 100% ili na wao waweze kupata masomo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ni namna gani bora mnayoitumia kwenye zile ajira zenu za muda, kwa sababu tumeona mara nyingi wanaoenda kufanya hizo kazi ni wazee na hawawezi kuzifanya kwa ufanisi? Mnafanya namna gani kuweza kuwapata ambao wanaenda kuzifanya hizo kazi za muda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Swali lake la kwanza, Serikali kupitia TASAF imeweka mkakati wa kuhakikisha watoto wanaotoka katika kaya maskini wanapewa kipaumbele kwa maana wanapewa mikopo kwa 100%, na kwa utaratibu huo TASAF imefanya makubaliano na imesaini hati ya makubaliano kati ya TASAF pamoja na Bodi ya Mikopo ili kuhakikisha kwamba wale watoto wanapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia hati ya makubaliano, TASAF imeendelea kuwapa kipaumbele wale watoto ambao wanatoka katika kaya maskini ili Bodi ya Mikopo iendelee kuwaona na kuwazingatia ili waweze kupata mikopo kwa 100%. Kupitia katika makubaliano hayo, TASAF pamoja na Bodi ya Mikopo imesaini makubaliano na katika makubaliano hayo, wamekubaliana na kuunganisha taarifa zao ili taarifa za TASAF ziunganishwe pamoja na taarifa ya Bodi ya Mikopo ili Bodi ya Mikopo waweze kuwapata kirahisi hawa watoto ambao wanatoka katika kaya maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hilo, taarifa ni kwamba, mwaka wa fedha 2025/2026 takribani watoto 5,958 wameweza kupata mikopo ya elimu ya juu, jumla ikifikia watoto 18,000 wameweza kufanikiwa kupata mikopo ya elimu ya juu ili waweze kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu kazi au ajira za muda. Serikali kwa kupitia TASAF imeweza kuweka mkakati mzuri namna ya kutoa ajira za muda kwa walengwa, hasa wale ambao tayari wako kwenye mfumo, na kwa kupitia hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza walengwa ambao tayari wameshasajiliwa katika kaya maskini waweze kupata kazi hizo za kujitolea au kazi za ajira za muda na hizi zinazotolewa ni mpango shiriki, kwamba jamii husika inashirikishwa ili kuwapata walengwa haswa ambao tayari wameshasajiliwa kwenye mfumo na tayari wanapatikana katika kaya maskini waweze kufanya kazi zile za ajira za muda.

Mheshimiwa Spika, kwa kupitia huko TASAF imeweka vigezo ambavyo vinatumika ili kuwapata wale washiriki. Kigezo mojawapo ni kuhakikisha kwamba washiriki wazingatie umri kuanzia miaka 18 mpaka 65, lakini kwa kuzingatia pia washiriki wale wanaoshiriki katika ajira za muda wawe na uwezo wa kufanya kazi kwa maana ya kuwa na afya njema na kigezo kingine ni kuhakikisha kwamba, wale washiriki ni wale ambao tayari waliosajiliwa kwenye mpango wa TASAF, ahsante. (Makofi)

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kutokana na umuhimu wa mradi huu, nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha wanapata mwekezaji haraka iwezekanavyo na huu mradi uweze kutekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa sekta ya uchukuzi ndio inachochea kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii. Ni namna gani sasa sekta hii inaweza kufanya kazi kwa haraka na kuhakikisha kwamba inapata wawekezaji wa ndani ili mradi huu uweze kutekelezwa kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Esther Malleko, kwa uzalendo wake na jinsi anavyofuatilia kwa ukaribu miradi ya uchukuzi lakini hasa pia uwanja wa ndege kule Kilimanjaro na Kaskazini kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishamjibu kwamba usanifu unaendelea. Nimhakikishie mara tutakapokamilisha, tumeshamaliza usanifu sasa tupo kwenye hatua ya kupata mkandarasi. Atupe muda, ninajua anatamani kuona kazi hiyo inaanza hata kesho. Tukishapata mwekezaji ambaye yuko tayari, tukishaelewana naye tutakuwa tayari kwa ajili ya kuanza kazi hii. Na nitoe rai, kwamba wawekezaji wa ndani na nje wachangamkie fursa hizi za kujenga hoteli kwenye viwanja vya ndege ili kuhakikisha sekta yetu inaboreka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu jinsi ambavyo tumejipanga kama sekta katika kuhakikisha kwamba tunashirikisha wawekezaji wa ndani katika uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi kwenye Taifa letu. Sote tunakumbuka mwaka jana tarehe 17 Julai, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Dira ya 2050. Katika dira hiyo ambayo kimsingi itaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2026 inasema tunataka tujenge Taifa kubwa la Tanzania ambalo litakuwa mfano katika ukanda wa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujenge Taifa kubwa ambalo uchumi wake kama ambavyo mnakumbuka Mheshimiwa Profesa Kitila mara kwa mara amekuwa akirudia ambayo itakuwa na uchumi wa dola trilioni moja, sasa hivi tunazungumzia uchumi wa karibu dola bilioni kama 87. Anasema tunataka tujenge Taifa ambalo wananchi kipato chao kitakuwa ni dola 7,000 sasa hivi unazungumzia kipato cha kama dola 1,200 au 1,300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ili tufikie azma hiyo, lazima sekta binafsi ipewe fursa ya kushika uchumi kwa sekta 70% kwa sababu hiyo, kama mnataka mjenge Taifa kubwa la namna hiyo ambalo 70% mmetoa kwenye sekta binafsi haukwepi kushirikisha wawekezaji binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama mnakumbuka wakati Mheshimiwa Rais anazindua dira yetu, alisema anataka mapitio ya sheria zetu za uwekezaji ambazo zinakwenda kulinda na kuhamasisha wawekezaji mbalimbali duniani, lakini mkazo ikiwa ni wawekezaji wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Esther Malleko kwamba Serikali inajipanga na nitumie nafasi hii kuwasihi wawekezaji wote wa ndani wachangamkie fursa katika miradi ya uwekezaji kwenye reli, kwenye viwanja vya ndege, kwenye SGR kuweka treni, kwenye bandari ili uchumi wa Taifa letu ushikwe na wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe rai kwa wawekezaji wa nje kwamba yapo manufaa makubwa wanayoyapata endapo wakija wakashirikiana na wawekezaji wa ndani ya nchi yetu. Kuna baadhi ya vitu ambavyo kimsingi wanapewa kupitia wenzetu wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mamba Kusini katika Jimbo la Vunjo imekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu ili tuweze kupata mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kata aliyoieleza Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Vunjo pia itahusishwa katika mkakati wetu wa Wizara, kwa sababu pia amesema kwamba ina changamoto kubwa. Ni kati ya zile kata ambazo na sisi tumepanga kwamba katika maeneo yenye changamoto kubwa tutayapa kipaumbele tunapoendelea na utekelezaji wa mkakati wetu huu wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kikubwa kwa Jimbo lake la Vunjo katika maeneo yote yenye changamoto kubwa, hasa wakati wa utekelezaji wa mkakati mahsusi wa Wizara wa hii miaka mitano tunayoendelea na utekelezaji wake. (Makofi)