MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za TASAF zinawafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Ahadi yangu kwake ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kujituma, na kwa uzalendo, ili malengo yaliyopangwa yafikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia program ya TASAF, imeweka mkakati mahususi wa kuhakikisha fedha/ruzuku zinawafikia walengwa kupitia matumizi ya mfumo wa malipo ya kielektroniki (e-payments) unaolenga kuongeza uwazi, usalama na ufanisi katika utoaji wa ruzuku kwa walengwa. Mkakati huo unatekelezwa kwa kutumia watoa huduma za kifedha walioidhinishwa ambao hulipa fedha moja kwa moja kwenda kwa walengwa kupitia akaunti zao za benki na mitandao ya simu.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu huondoa utaratibu wa kutuma fedha taslimu, na hivyo kupunguza mianya ya upotevu, ucheleweshaji au matumizi yasiyo sahihi ya fedha. Pili, malipo yote hufanyika kwa kuzingatia taarifa za walengwa zilizohakikiwa katika mfumo wa usimamizi wa walengwa, Management Information System (MIS), ambapo kila mlengwa hulipwa kulingana na utambulisho wake wa kipekee, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa hoteli katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uandaaji wa pembuzi yakinifu ya ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro. Kwa sasa taratibu za kutafuta mwekezaji wa ujenzi wa hoteli zinaendelea.