MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninapenda kuuliza swali. Ni lini Kituo cha Afya cha Kata ya Rwamgasa kitakamilishwa na kuanza kutoa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika katika Kituo cha Afya cha Rwamgasa na kiukweli kimeanza kutoa huduma za OPD na kuna majengo yanazidi kuongezwa pale kupitia mbia wetu wa Buckreef, na majengo haya yanakwenda kukamilika ndani ya mwezi wa tatu na kuanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa maelekezo mahususi kwa Mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu katika ujenzi wa majengo haya ili akina mama wetu wanaojifungua zaidi ya 200 mpaka 250 kwa mwezi waweze kupata huduma hii ya afya ya msingi. (Makofi)