Supplementary Questions from Hon. Tinnar Andrew Chenge (5 total)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Chenge Sekondari iliyopo Kata ya Somanda pale Bariadi ilijengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2016, na kuna maabara ambayo ni two in one, lakini tangu kipindi hicho shule hiyo na maabara hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha maabara hiyo ili kuunga mkono juhudi za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza Serikali inatambua mchango mzuri wa wananchi wa Jimbo la Bariadi na Bariadi Mjini kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Secondari ya Chenge. Nakuhakikishia kwamba, Serikali ilishafanya tathmini, na tunayo orodha ya shule zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zote ambazo zimejengwa kwa fedha ya Serikali, kwa maana ya Halmashauri, yaani Serikali Kuu, tayari tunafahamu upungufu wa majengo na miundombinu inayohitajika. Tunaendelea na taratibu za fedha, ili tuweze kupeleka kukamilisha shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Shule ya Sekondari ya Chenge itapewa kipaumbele. Itapelekewa fedha ili tuhakikishe miundombinu hiyo inakamilishwa.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kumekuwa na changamoto ya kukatikakatika umeme katika Mkoa wa Simiyu, na Serikali iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme. Je, ujenzi huu umefikia hatua gani? Lini utakamilika ili kuondoa changamoto hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia namna ambavyo Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza majukumu ya ujenzi wa substation katika eneo la Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inaendelea na mpaka sasa ujenzi wa substation umefika zaidi ya 30%. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira. Ninamhakikishia mara baada ya substation hiyo kukamilika, Mkoa wa Simiyu utakuwa umeondokana na changamoto ya kukatikakatika kwa umeme. Ahsante.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Shule ya Sekondari Busangwa iliyopo Kata ya Sakasaka katika Jimbo la Kisesa ina wanafunzi wa kike takribani 250, lakini hakuna mwalimu wa kike hata mmoja. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nipokee hoja ya Mheshimiwa mama yangu, Mheshimiwa Mama Chenge, lakini nitoe tu ufafanuzi ili kuweka rekodi sawa kwamba tunafahamu umuhimu wa walimu wa kike katika shule zetu zote za wanafunzi wa kiume na wa kike. Tunafahamu pia kuna mahitaji maalum ambayo mara nyingine ni vizuri mwalimu wa kike akiwa katika shule hizo. Kwa hiyo, suala hilo tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu, ninaomba kuulizwa swali la nyongeza. Ni lini Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Afya cha Bunamhala Wilaya ya Bariadi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza kuhusu Kituo cha Afya Simiyu, Bariadi. Katika vile vituo vyetu vya kimkakati Majimbo 94 na yale Majimbo mapya pamoja na Halmashauri ya Wilaya Simiyu na wao ni wanufaika, watakwenda kupata kituo cha afya. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni sera ya Serikali kuhakikisha kwamba kila makao makuu ya mkoa yanaunganishwa na mikoa jirani kwa barabara za lami. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Bariadi na Gangabilili – Mwanhuzi – Sibiti - Iguguno na Singida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hili swali linafanana na swali la msingi kwa sababu ndiyo barabara ambazo zinatakiwa zijengwe zote. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kwa awamu hii tumepanga kujenga kiwango cha lami kilometa 50 katika hiyo barabara ya Bariadi – Sibiti kuja Singida.
Mheshimiwa Spika, tayari tuna mkandarasi, na tunachosubiri ni kulipa malipo ya awali ikiwa ni pamoja na kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika lile daraja la Sibiti ambapo kutakuwa na upande wa Sibiti kwa maana ya Simiyu na upande wa Singida, ahsante.