Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyetujalia sote kuwa na afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, hii ni mara yangu ya kwanza kusimama, ninaomba uniruhusu nichukue nafasi hii kuishukuru Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kuteua jina langu kuwa Mbunge wa Viti Maalum, kuwakilisha Wanawake wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee, ninaomba pia, niwashukuru wapiga kura wangu, Wanawake wa Mkoa wa Simiyu, kwa heshima kubwa waliyonipa. Nawaahidi kuwa nitawatumikia kwa moyo wangu wote. Mwisho, japo siyo kwa umuhimu, naomba nimshukuru mume wangu, familia yangu, pamoja na wapiganaji wangu kwa support yao kubwa sana katika safari yangu ya kisiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutuletea maendeleo. Mimi, kama mwanamke, ninatoka Mkoa wa Simiyu, nasema ahsante sana kwa Mradi mkubwa wa Maji, Ziwa Victoria, ambao ametuletea sisi wananchi wa Mkoa wa Simiyu wenye gharama ya shilingi bilioni 440. Mradi huu ukikamilika, hakika utaleta tabasamu kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na hususan wanawake ambao ndiyo wahanga wakubwa wa tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba, kwa ziara zake anazofanya katika mikoa. Ninamwomba na sisi atutembelee, Mkoa wa Simiyu kwa sababu, tunaona tija ya ziara zake, lakini pia, kwa hotuba nzuri ambayo imeleta matumaini kwa wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, ninaomba sasa niweze kuchangia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira pamoja na Mahusiano kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, ndugu yangu Mheshimiwa Deus Sangu, pamoja na wasaidizi na watendaji wake kwa kazi kubwa ya kusimamia Wizara hii kwa kiwango na weledi mkubwa sana. Mchango wangu ninauelekeza kwenye eneo la mafunzo ya uanagenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kimojawapo cha mafunzo haya ya uanagenzi ni makusanyo ya Mfuko wa SDL ama Skills Development Levy. Kwa Mwaka 2023/2024 Serikali ilikusanya kiasi cha shilingi 358,924,000,000 na katika fedha hizi shilingi 119,641,000,000 zilipaswa zipelekwe kwenye mafunzo ya uanagenzi, lakini kiasi kilichopelekwa ni shilingi bilioni tisa tu, sawasawa na asilimia sifuri, nukta sifuri saba tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka uliofuata pia, kiasi kilichokusanywa kilikuwa ni shilingi 233,568,000,000 ikiwa pia, ni pungufu ya kama shilingi 125,356,000,000 ukilinganisha na kipindi kilichopita. Baadaye nitaomba Wizara inayohusika itueleze ni kwa nini kumekuwa na poromoko kubwa namna hii la makusanyo haya?
Mheshimiwa Naibu Spika katika kipindi hicho pia, fedha zilizopaswa kupelekwa katika Mfuko huu wa Mafunzo ilikuwa ni shilingi 700,858,000,000, lakini zilipelekwa shilingi 10,0800,000,000 tu, ikiwa ni sawasawa na asilimia sifuri nukta sifuri moja tatu nane.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa ya Utekelezaji ya Awamu ya Nane ya Mafunzo ya Uanagenzi, kama ilivyoletwa kwetu kwenye Kamati na Wizara husika, ilitufahamisha kwamba, kuna vyuo 100 ambavyo vilikuwa vimeomba kutoa mafunzo haya ya uanagenzi, lakini kutokana na changamoto ya rasilimali fedha ni vyuo 46 tu ambavyo viliweza kupata nafasi ya kutoa mafunzo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo hivi pia vilikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi takribani 16,000 na ushee, lakini kutokana na tatizo la rasilimali fedha, viliweza kudahili vijana 5,746 tu, ikiwa ni 34.415%. Vyuo hivyo vya uanagenzi ni muhimu sana katika kutoa mafunzo stadi kwa vijana wetu. Sasa kama kweli tuna nia ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, ninaiomba Serikali yangu sikivu iangalie kipengele hiki kwenye vyuo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wetu wengi sasa hivi wanakaa kwenye mitandao waki-bet, lakini kama wangeweza kupata mafunzo stadi haya ninaamini kabisa yangewasaidia kujiajiri na kuweza kuajiriwa. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu sikivu iliangalie eneo hili kwa jicho la tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitakuwa ni kitu cha ajabu sana kama tutakuwa tunapeleka vijana hawa kwenye mafunzo halafu tukitoka tunawarudisha mitaani ambako hakuna ajira. Kwa hiyo, ninaomba fedha hizi za Mfuko wa SGN ikiwezekana zitumike katika kununua vitendea kazi na kuwakabidhi vijana hawa wanapomaliza mafunzo yao ya uanagenzi. Ninaamini kabisa tukifanya hivi tutakuwa kwa kiasi kikubwa sana tumetatua tatizo hili la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la uchangiaji lilikuwa ni hilo, lakini ninaomba niungane na Wabunge wenzangu pia kuiomba Serikali iipatie TARURA fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara nyingi ambazo zimeharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Sasa ninaomba niishukuru Kamati yangu ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Hawa Mchafu pamoja na Makamu wake, kwa jinsi ambavyo tunafanya kazi kama timu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)