Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yannick Ikayo Ndoinyo (1 total)

MHE. YANNICK I. NDOINYO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo ya malisho kutoka hekta milioni 3 mpaka 6 kama Ilani ya CCM inavyosema?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Yannick Ikayo Ndoinyo, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kutekeleza maelekezo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025/2030 na Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa kufungua rasmi Bunge la Kumi na Tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma, tarehe 14 Novemba, 2025 kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali itaongeza maeneo yaliyopimwa na kutengwa kwa shughuli za ufugaji kutoka hekta milioni 3.49 hadi hekta milioni sita.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara, Idara na Taasisi zenye majukumu ya kisheria ya kupanga na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi, tumeanza kuandaa mkakati wa miaka mitano wa kutenga hekta milioni 2.51 kwa ajili ya shughuli za ufugaji. Wakati wa utekelezaji wa mkakati huu, Waheshimiwa Wabunge wote watashirikishwa.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.