Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Salome Wyckiffe Makamba (2 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Mtambo wa Refinery wa kuchakata Mafuta kwa kuwa Mradi wa Bomba la Mafuta toka Uganda unatarajia kuanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Msheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Abbas Gulam, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa EACOP unatekelezwa na wawekezaji binafsi (private investors) kwa kushirikiana na Serikali za Uganda na Tanzania. EACOP Ltd ni kampuni inayosimamia ujenzi na baadaye uendeshaji wa miundombinu ya mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wamepanga kujenga mtambo wa kusafisha mafuta ghafi (refinery) kwa upande wa Uganda ambao utachakata mafuta, ambayo yatatosha soko la Uganda na nchi jirani, ikiwemo Tanzania. Naomba kuwasilisha.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kusafisha mafuta ghafi yanayotoka Uganda kupitia Bomba la Mafuta EACOP?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ninaomba kujibu swali namba 87 la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa Tanzania kwenye mradi wa bomba la EACOP upo kwenye biashara ya kusafirisha mafuta ghafi tu, yaani transit nation kutoka Kabaale – Hoima hadi Chongoleani – Tanga na baadaye kupelekwa kwenye masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba ya mauzo ya mafuta hayo imeshaingiwa tayari kati ya wabia wa mkondo wa juu nchini Uganda, yaani up streamers ambao ni Serikali ya Uganda na makampuni ya Kimataifa ya Total Energies kutoka Ufaransa na CNOOC kutoka China kwa kuzingatia vigezo vya usanifu wa kitaalamu na uwezo wa uzalishaji wa visima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ifahamike kwamba kwenye biashara hii tayari mikataba ya mauzo ya mafuta haya imeshaingiwa kati ya wabia wa mkondo wa juu na wanunuzi wa masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.